UCHAMBUZI: Uko wapi ukali wa Rais Magufuli?

Salim Nyomolelo

Mimi ninamuita Rais John Magufuli, wengine humuita Jembe la Chato, wengine Tingatinga, wengine humuita Mtumbua majibu, wengine Kiboko ya mafisadi, wengine Rais wa wanyonge. Kila mwananchi ana namna ya kumtaja Rais Magufuli kwa namna alivyomgusa katika utendaji wa kutatua kero za wananchi na kuwawajibisha viongozi wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo. Majina haya yote yanaashiria uimara wa mtu katika kufanya kazi na kutenda haki.

Kule kwetu Iringa wakati wa utawala wa machifu, viongozi kama Rais Magufuli walikuwa wakifanyiwa matambiko katika miti na mawe makubwa na kuidhinishwa kula nyama ya mbwa ili kuwafanya kuwa imara zaidi, nyama ya mbwa ilikuwa ikiliwa hasa na machifu ama viongozi wengine ikiwa imechanganywa na dawa nyingine za asili ili kuwaongezea viongozi uimara na ujasiri wa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maeneo yao ya utawala.

Ukoo wetu wa Nyomolelo ni zao la Uchifu Mwadasi ambaye ni babu wa baba yangu, alikuwa chifu akibebwa na machela na watumwa na chakula chake kikubwa kilikuwa nyama ya mbwa. Watumwa walikuwa wanakula nyama ya ng’ombe, mbuzi ama kuku lakini si nyama ya mbwa.

Wakati mwingine mtumwa ama mtu wa kawaida akionekana anakula nyama ya mbwa aliuawa. Nyama ya mbwa ilikuwa na heshima. Kwa zama zile za zamani, Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi alistahili heshima ya kula kitoweo hicho.

Huwa namsikia Rais akirudia kauli yake mara kwa mara akisema baadhi ya wateule wake hawajamwelewa jambo linalosababisha kufanya mambo ambayo si tija kwa taifa. Binafsi huwa namwelewa akisema hivyo na wewe msomaji pia utakuwa unamwelewa ama utamwelewa baada ya kumaliza kusoma makala haya.

Kitendo cha idadi kubwa ya wananchi kuzielekezea kero zao moja kwa moja kwa Rais ili azitatue ikiwa katika maeneo hayo kuna viongozi kuanzia ngazi za kijiji ama mtaa, kata, wilaya, mkoa na hata wizara ni ishara tosha kuwa Rais hajaeleweka na viongozi hao, anataka kero za wananchi zishughulikiwe na wateule wake.

Wananchi hufikia hatua hii baada ya kero zao kushindwa kutatuliwa kwa muda mrefu. Hawa humwita Rais Magufuli ni Rais wa wanyonge kwa sababu kero zao zimesikilizwa bila kutatuliwa na wateule wake na hivyo kimbilio pekee ni yeye Rais.

Tumeona Rais Magufuli akifanya ziara maneneo mbalimbali nchini huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kumsikiliza na kueleza malalamiko yao ambayo yanawahusu viongozi ama yanahusu kero zao lakini cha kushangaza kero hizo zimeshindwa kutatuliwa ngazi za chini za uongozi na wananchi kuamua kumfikishia Rais ili azitatue. Hawa humuita Rais, Jembe la Chato

Katika ziara zake tumekuwa tukisikia watoa malalamiko walivyojitihadi kufuatilia kero zao bila mafanikio wakimueleza Rais lakini pia tumesikia namna viongozi wanavyoshindwa kusimamia miradi ya maendeleo ambapo baada ya kufikishiwa malalamiko ya kusuasua kwa miradi hiyo Rais Magufuli hutoa maagizo papohapo ili kuleta tija. Hawa humuita Rais Magufuli Tingatinga. Tingatinga kwa kuwa hashindwi na jambo lolote kutokana na sifa ya tingatinga kuwa na uwezo wa kupasua miamba na kuangusha miti mikubwa.

Pamoja na hayo, kero kubwa ya ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya viongozi, Rais ameishughulikia ipasavyo. Mafisadi na wala rushwa wanashughulikiwa. Wananchi ambao wameguswa na jambo hili wanamtaja Rais Magufuli kama kiboko ya Mafisadi.

Rais pia amekuwa akifanya mabadiliko kwa baadhi ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa mikoa, viongozi waandamizi wa taasisi za serikali na mawaziri kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo. Wengine huwaondoa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka, ubadhilifu na rushwa.

Wananchi wengi huguswa na hatua hii ambayo Rais Magufuli huichukua dhidi ya watendaji wabovu. Kwa jambo hili wananchi humtaja Rais Magufuli kuwa ni mtumbua majibu. Rais humfananisha mtendaji mbovu anayeisababishia serikali hasara sawa na jipu ambalo likiachwa bila kutumbuliwa litaongeza madhara zaidi.

Rais Magufuli anawateua watendaji, anawapa nyenzo zote za kufanya kazi ya kusimamia miradi, kubuni miradi mipya ili kuongeza mapato ya serikali, kutatua kero za wananchi kwa wakati ili kuleta tija na maendeleo. Rais Magufuli anataka wananchi wasikilizwe, washughulikiwe kero zao lakini baadhi ya viongozi hawafanyi hivyo na badala yake wanakuwa wao ndio kero kwa wananchi. Viongozi hawa wakitumbuliwa wanamuita Rais Magufuli ni mkali.

Kwangu Rais Magufuli si mkali, ila ni mzalendo kwa nchi yake, mzalendo kwa rasilimali kwa wananchi wake, ni kiongozi ambaye anawapenda wananchi wake, ni kiongozi imara katika kushughulikia kero za wananchi pamoja na kushughulika na viongozi ambao ni kero kwa wananchi kutokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa mujibu wa miongozo ya kazi zao.

Ukali wa Rais Magufuli uko wapi? Kuwasimamisha kazi viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya? Kuwatumbua mafisadi na wala rushwa? Je tunataka awaache viongozi wasiowajibika? Tunataka awaache viongozi wanaoshindwa kusimamia miradi ya Serikali ikiwamo mabilioni ya fedha?

Tunataka Rais asiwachukulie hatua watendaji wasiofuata sheria na kutanguliza uzalendo katika majukumu yao? Ama kitendo cha kuchukua hatua kwa watendaji wabovu ndio ukali na si uwajibikaji?

ngozi jasiri na mwenye misimamo kwa kutanguliza maslahi ya anaowaongoza bila kupendelea wala kubagua, kiongozi asieangalia rafiki ilimradi amekosea anamwajibisha ni kiongozi ambao wanastahili heshima kubwa, heshima ya kuongezewa ujasiri zaidi wa kuendelea kukabiliana na kero za wananchi na kero viongozi. Rais Magufuli ingekuwa anaongoza wakati ule wa enzi za uchifu kule kwetu mkoani Iringa, alistahili kupewa heshima kubwa, heshima ya kula kitoweo cha nyama ya Mbwa, tena aliyenona na mkali. Mungu akubariki Rais wetu

Kwa maoni 0754654410