MAONI: Ushauri wa Kikwete upewe nafasi Afrika

Kauli kwamba Umoja wa Afrika (AU) umefanikiwa katika malengo yake ya kuleta uhuru lakini ukiwa na changamoto kubwa za kukosekana utawala bora, umaskini na maradhi, inastahili kufanyiwa kazi haraka.

Kauli hiyo iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete katika tamasha la 11 la kitaaluma la Mwalimu JK Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inapaswa kupewa kipaumbele na nchi zote ili kuleta maendeleo ya kweli ya Bara la Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, Kikwete ambaye alikuwa mhadhiri wa heshima katika kongamano hilo, alisema, “kumekuwa na changamoto zinazohitaji kuangaliwa ambazo ni kuwapo kwa sheria kandamizi, ushiriki usioridhisha wa wananchi, kutokuwapo kwa uhuru wa habari na kwa mikakati ya kupambana na rushwa.”

Tunaungana na Kikwete kwa kuwa tunaamini kwamba, “kama watu wa Afrika, hatuna njia nyingine, bali kutatua hizi changamoto kama zilivyoelezwa.”

Hata mfano aliotoa kuhusu mpango wa kujitathmini kiutawala bora (APRM) akihoji iwapo viongozi wa Afrika walikuwa wakisikiliza maoni ya wengine kuhusu utawala bora, uko dhahiri, unaotoa sura kwamba suala la utawala bora limeendelea kuwa donda ndugu katika nchi nyingi.

Masuala anayoyaibua Kikwete ni mambo ya kawaida katika nchi za Afrika lakini viongozi wengi wa bara hili wanatamba kwamba wanayotekeleza “ndiyo demokrasia ya Afrika.”

Mathalan, ni jambo lisilo na kificho kwamba Afrika imekuwa mfano wa kudumu wa dunia, ambao viongozi wake wengi hubadili katiba za nchi zao ili waendelee kusalia madarakani bila ukomo.

Si hayo tu, lakini pia ili ajenda zao za kukandamiza demokrasia ziweze kutekelezeka, viongozi wengi hukandamiza uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari.

Katika nchi nyingi, taarifa zinabainisha kupungua ushiriki wa wananchi katika masuala ya demokrasia, kama vile uchaguzi kutokana na ama kukatishwa tamaa au kutishwa ili viongozi waweze kufanya yale wanayokusudia kwa masilahi yao.

Kwa upande wa sheria, hili nalo halina ubishi kwa kuwa hakuna kinachoshindikana katika baadhi ya nchi ambako sheria hutungwa za kuwaneemesha watu wachache na kuwakandamiza walio wengi.

Jambo jingine ambalo tunadhani Kikwete ameliona na ni la muhimu, ni kutokuwapo mikakati ya kupambana na rushwa kati nchi nyingi. Pia katika baadhi ya nchi, hata zenye kupambana na rushwa, hatua zinazochukuliwa huwalenga baadhi ya watu hasa wa chini na kuwaacha wengine kulingana na matakwa ya watawala.

Tungependa kushauri kuwa maneno ya Kikwete ambayo yalitolewa katika mimbari yenye fursa ya kusikika kimataifa, yachukuliwe kwa uzito wake na kufanyiwa kazi. Ifike wakati Afrika iungane katika mtazamo Kikwete na kuanza kupaa kwa pamoja.

Tuanze sasa kujiuliza, hivi inakuwaje teknolojia zinabadilika, miji inakua, elimu inaongezeka lakini fikra za ubinafsi na ukiukaji kanuni za utawala bora zinabaki palepale?

Inabidi pia tujiulize, inakuwaje, katiba na sheria kandamizaji Afrika zinabaki kuwa ni zilezile au zinaongezwa ukali wakati mambo mengine yanazidi kubadilika kuwa bora zaidi?

Hapo ndipo tunasema ushauri wa Kikwete upewe nafasi na mataifa yote katika Bara la Afrika.