UCHAMBUZI: Uzalendo ni kiboko ya ufisadi

Katika miaka ya 1960, Mfalme wa Ethiopia aliwataka Wazungu waache kusambaza uvumi kuwa walikusudia kuondoa makovu ya biashara ya utumwa na ukoloni viliyoiathiri Afrika.

Aliwaeleza wazi kuwa wasingeweza kamwe kurudisha damu waliyoimwaga wakati huo, kuzirudisha koo na familia walizozitawanya, kurudisha mamilioni ya tani za dhahabu, pembe na tunu kemkem walizotorosha, wala hawawezi kuurudisha utamaduni wa Mwafrika baada ya kuusigina kwa zaidi ya karne.

Alipoona kuwa wameng’ang’ana wakidai kutaka kuleta haki sawa aliwakubalia kwa sharti moja tu: kwamba kwa sababu wamewekeza katika Elimu na Afya katika bara zima la Afrika, sasa watoe Elimu sawa kwa watoto wote. Yaani watoto wa Kiafrika waruhusiwe kusoma kwenye shule wanazosomeshwa watoto wa Kizungu.

Wazungu walilikataa katakata jambo hilo na kudai kuwa ilikuwa ni mapema mno kutekeleza hilo. Hila yao ikagundulika kuwa ilikuwa ni kuudanganya umma wa Waafrika kwa misaada ya chakula na nguo ili waaminiwe kuwa wanathamini usawa, kisha waendelee kukombeleza hata kidogo kilichobaki.

Binadamu wote ni sawa na kila mmoja anastahili heshima. Ni haki yake ya msingi kibinadamu, kikatiba na hata kiimani. Hakuna aliyemzidi mwenzie katika haki hata kama ana mwili, nguvu, akili au uwezo wa ziada. Pia haki inatengua tofauti ya madaraja yanayozingatia rangi, kabila, dini, utaifa na itikadi.

Adui namba moja wa haki ni rushwa. Rushwa kwa mujibu wa Kamusi huru ya Wikipedia ni aina ya mwenendo usio wa uaminifu au usiofaa kwa mtu aliyepewa mamlaka, akatumia nafasi hiyo ili kupata faida binafsi.

Ni kukosa uaminifu na kutumia vibaya mamlaka uliyopewa. Ni matumizi yasiyo halali ya ofisi au madaraka kwa ajili ya kujinufaisha mwenyewe. Ni kutumia nafasi ya ya uongozi au ofisi kwa manufaa binafsi badala ya kutumikia umma. Kwa ujumla ni msukumo wa kupotosha haki.

Rushwa inaweza kuwa ya fedha, mali, ngono au nafasi. Katika nchi inayoendeshwa kwa rushwa, daima wenye fedha ndio wanaokuwa na haki. Masikini, wajane na yatima huwa takataka mbele ya wenye fedha kiasi kwamba wanaweza kuwaamulia hatima yao. Mambo haya yalikuwepo tangu enzi za Manabii na tunasoma jinsi Mwenyezi Mungu anavyoilaani rushwa.

Swahiba mkuu wa rushwa ni ufisadi. Huu ni mwenendo wa mtu kujitwalia mali ya umma kwa manufaa yake binafsi. Kwa lugha nyepesi ufisadi ni uroho, ulafi, umero wa mali ya umma. Kwenye baadhi ya nchi dhambi ya ufisadi imewekwa kwenye daraja sawa na uuaji, na adhabu yake ni kunyongwa ama kupigwa risasi hadharani.

Ufisadi unaweza kuhusisha shughuli nyingi ikiwa ni pamoja na rushwa, matumizi mabaya ya amana ya Taifa au rasilimali za nchi na udhalimu. Mafisadi walioachiwa nafasi walijenga uwezo wa kujikinga na sheria na hata waliweza kushika hatamu za Serikali zao.

Nchi zote zilizopigania haki za raia wake, zilipiga vita rushwa na ufisadi. Ziliweka miiko thabiti ya uongozi ili kuwaepusha na kishawishi cha ubadhilifu. Waliapizwa kwa viapo vikali vya kutokutoa wala kupokea rushwa katika hali yoyote, na kuchukulia cheo kama dhamana na si mali yao.

Mafisadi ni watu wanaopenda kuabudiwa. Hawawezi kuheshimu fursa sawa kwa kuogopa heshima sawa. Wangependa wao na jamaa zao wapate elimu, tiba na huduma zote kwa daraja la juu wakiuacha umma ukikosa hata daraja za chini.

Mataifa yote yaliyofanya vizuri katika ulinzi wa haki, utawala wa sheria na vita dhidi ya ufisadi yaliweka misingi katika uzalendo. Yalianza kuwajenga watoto na vijana wadogo kiasi kwamba walipokomaa waliendesha nchi wakiwa na uchungu na mali ya umma.

Chipukizi, skauti, mgambo na Jeshi la Kujenga Taifa ni mifano ya makundi ya kizalendo yaliyopata kujengwa Tanzania. Makundi kama hayo yangali yakiendelezwa huko Uchina na Israeli. Matunda yake yanaonekana kwa nchi hizo kukuza uchumi maradufu.

Kwa mtazamo wangu suala la uzalendo linaweza kuibuliwa upya na nchi yetu kujenga uchumi wa kati na wa juu baada ya muda mfupi sana. Ukirudi nyuma kwa miaka thelathini viongozi wengi wa leo walikuwa bado mashuleni. Ninamaanisha kuwa tukilifufua leo, miaka thelathini ijayo tutakuwa na viongozi wazalendo halisi.

Nadhani kuna haja ya kupitia upya mitaala yetu. Pamoja na kuzingatia masomo ya kiada, shule zetu zinaweza kuongeza nafasi ya masomo ya ziada kama ilivyokuwa kwenye nyakati zilizopita. Masomo kama ya sanaa na michezo yaliwakutanisha wanafunzi wa kada tofauti katika jambo moja, hivyo ilikuwa rahisi kuwajenga kizalendo kwa pamoja.

Ikumbukwe pia sanaa na michezo iliwakutanisha wanafunzi kutoka ngazi ya kata, wilaya, mkoa hadi Taifa kwenye mashindano. Sote tunakumbuka Umishumta na Umiseta zilivyopasua anga hadi Kimataifa. Huu ndio wakati ambao wanafunzi wanaweza kujadili uzalendo kwa mapana yake.

Jambo lingine ni mihadhara au midahalo (debating). Pamoja na kumkomaza mtoto katika fasihi, lakini midahalo huongeza chachu kwa wanafunzi kulingana na mada ya siku. Mada za kizalendo zinaweza kuongeza upeo wa kujitambua miongoni mwa wachangiaji.