Video na picha za mitandaoni huwatambulisha vizuri wasanii

Saturday May 25 2019Tumaini Msowoya

Tumaini Msowoya 

By Tumaini Msowoya

Kati ya vitu vinavyofanya mtu atamani kutizama na kusikiliza kazi ya msanii yeyote yule ni muonekano wake.

Muonekano wa msanii siyo tu mpaka kwenye matamasha, bali huonekana hata katika akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Wapo baadhi ya wasanii makini walio weza kupiga picha na video zenye mvuto na kutupia katika mitandao mbalimbali ya kijamii lakini wapo wale wasiojali hilo.

Hawa wasiojali wao huokota picha yoyote hata yenye ukungu aliyopiga wakati wametoka kuamka na kuitundika kwenye akaunti yake bila wasiwasi.

Kwa dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia si kazi rahisi kumfahamu msanii yeyote.

Utembelee kwenye kurasa zake za facebook, twiter, youtube, istagram na nyingine ndipo utamfahamu vizuri.

Advertisement

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Audrey Azoulay katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya urithi wa sauti na picha aliwahi kusema vitu hivyo ni urithi kizazi hadi kizazi.

Kwa maana nyingine, picha hizo ni urithi utakaodumu kizazi hadi kizazi na jamii yako itaendelea kujivunia wewe.

Kwa maana hiyo ujumbe wangu leo ni kwa ajili ya wale wasiojali na wasiojua kama picha na video wanazoweka mitandaoni ni utambulisho wao muhimu.

Wakati mwingine unaweza kutafuta picha au video ya msanii fulani ili ujue nini anafanya, kazi gani mpya ameleta au mikakati yake ukaishia kupata vituko.

Mhariri wa Burudani Mwananchi, Julieth Kulangwa aliwahi kuniambia kwamba picha kali inamfanya mwandishi kutafuta jambo zuri la kumuandika msanii hiyo.

Yaani unapopiga picha nzuri au kuweka video kali kwenye mitandao ya kijamii unawahamasisha watu kujua zaidi kuhusu kazi zako.

Kuna baadhi ya ndugu zangu waimbaji wa muziki wa Injili ambao huhisi dhambi kuwa na picha kali kwenye mitandao wakidhani hayo ni ya dunia.

Hapana. Jitambulishe wewe ni nani na unafanya nini?

Kwa kufanya hivyo utawapa unafuu kupata picha yako wanapokutana na jambo lako jipya.

Si hivyo tu, ukiweka picha na video nzuri utavutia taasisi na kampuni mbalimbali zikiwamo za matangazo ya biashara kutaka kufanya kazi na wewe.

Hivi unadhani kwa nini baadhi ya wasanii huchaguliwa kuwa mabalozi wakiwakilisha bidhaa, kampeni au jambo lolote, unadhani moja ya kigezo ni hizo picha na video zenye ukungu?

Ni vizuri kujifunza kwa wasanii walioweza kuvuka hatua hiyo.

Jambo la msingi la kujua ni kwamba popote unapokuwa na chochote unachofanya mradi kisiwe binafsi ‘pesonal life’ wapo wanaokutazama kama ‘role model’.

Kwa maana hiyo jiweke kwenye mtazamo mzuri na picha utakazopiga zitabaki kuwa kumbukumbu njema ya jambo hilo vizazi na vizazi.

Popote unapokuwa na chochote unachofanya kumbuka wewe ni kioo cha kujitazamia. Watu watapenda wakuone nao wajifunza.

Ubunifu ni pamona na kupiga picha kali tena sio kwa nguo uliyowahi pigia juzi.

Hata siku moja usikubali kupigwa picha wakati ukiwa na matongo tongo umetoka kuamka.

Ukitaka kupiga picha hakikisha umependeza na unavutia ndipo uruhusu picha zako zisambazwe kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Jambo la muhimu kwa wasanii ni kukumbuka kwamba wao ni kioo cha jamii.

Picha zisizo na maadili zinawavunjia heshima na kuifanya jamii iliyokuwa inawaheshimu kuanza kuwadharau.

Mathalani, watu walipenda nyimbo zako mara wanaingia kwenye mtandao wanaona mavazi yako ni nusu uchi.

Unadhani nini kitatokea? Ni kuwapoteza kiasi kwamba hata ukija na kazi mpya haithaminiwi tena.

Msisahau kwamba mitandao haisahau. Siku yoyote ukiwa na jambo la maana na ukataka kuishirikisha jamii ujumbe wako hautapokelewa na badala yake watu wataanza kufukua makaburi kwa kuanza kuposti picha zako za zamani ulizopiga bila maadili.

Kila mtu anataka mafanikio na anazo ndoto za kuwa kwenye nafasi ya juu zaidi siku zijazo.

Unaweza kufikia ndoto yake na ukaendelea kuheshimika kwa kupiga picha na video nzuri kisha kuziweka mtandaoni ili kila anayekutafuta ajifunze jambo jema toka kwako.

Usisahau kwamba wewe ni barua ya kusomwa na watu wote.

Ujumbe wako kwenye hiyo barua lazima mtu anayesoma asome kwa tabasamu mwanana.

Kuwa mfano wa kuigwa kwa kupiga picha na video kali, zenye maadili mazuri na kuziweka mitandaoni ili usiwape tabu wanaotaka kujifunza kupitia wewe.