MAONI: Vyama vya michezo vijipange kwa Olimpiki

Monday October 28 2019

 

Michezo ya Olimpiki imepangwa kuanza Julai 24 mpaka Agosti 9 mwakani nchini Japan. Tanzania ni miongoni mwa mataifa 206 yanayotarajiwa kushiriki katika matukio zaidi ya 339.

Tanzania itashiriki michezo ya Olimpiki baada ya kushinda medali mbili za fedha mwaka 1980 Moscow nchini Russia, zilizoletwa na wanariadha, Selemani Nyambui katika mbio za mita 5,000 na Filbert Bayi mita 3,000 kuruka viunzi na kukanyaga maji.

Mpaka sasa wanariadha wa Tanzania waliofuzu ni Alphonce Simbu na Failuna Abdi watakaokimbia mbio za marathoni (kilomita 42) ambazo ni moja kati ya matukio 339 yatakayofanyika.

Timu ya judo inasubiri nafasi za upendeleo kufuatia kushindwa kutamba katika mashindano ya dunia ya kufuzu yaliyofanyika hivi karibuni nchini Japan.

Ngumi ambayo imekuwa ikishiriki Olimpiki hakuna kinachoendelea katika maandalizi ya kufuzu. Timu ya kuogelea imepata nafasi ya kushiriki Olimpiki kwa nafasi za upendeleo.

Baadhi ya michezo 42 inayofanyika katika Olimpiki ni soka, baiskeli, kikapu, wavu ya ufukweni, makasia, gofu, magongo, mpira wa mikono, judo na kuogelea.

Advertisement

Pia imo tenisi ya meza, taekwondo, tenisi, mpira wa wavu, kunyanyua vitu vizito na kulenga shabaha ambapo tumeona nchi nyingi zikipeleka idadi kubwa ya wanamichezo kwenda kushindana.

Hata hivyo, Tanzania imeshindwa kutumia fursa hiyo kupeleka idadi ya kutosha ya wanamichezo badala yake imekuwa ikiwakilishwa na wanariadha tu. Mara ya mwisho katika michezo ya Rio 2016 Brazil, Simbu alimaliza wa tano katika mbio za marathoni na Tanzania iliwakilishwa na wanamichezo saba, wanariadha watano, muogeleaji na mchezaji judo.

Afrika Kusini msimu uliopita ilikuwa na wanamichezo 137, Kenya (89), Ethiopia (34), Misri (120), Cape Verde (watano), Lesotho (wanane), Burundi (tisa), Rwanda (wanane) Uganda (21), Marekani (554), Hispania (306), Urusi (282), Ujerumani (425) na Australia (421).

Kitendo cha nchi hizo kupeleka wanamichezo wengi ni ishara kwamba vyama vyao vya michezo vilifanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya wanamichezo wao.

Wakati nchi hizo zikiwa katika maandalizi ya kupeleka idadi kubwa ya wanamichezo wao, hapa kwetu hali ni tofauti tena washiriki wake wakiwa wachache.

Licha ya Olimpiki kushirikisha michezo tofauti 42, Tanzania imekuwa ikiwakilishwa zaidi na mchezo mmoja wa riadha.

Kitendo cha nchi kupeleka wanamichezo wachache kinaonyesha namna viongozi wa vyama vya michezo wasivyokuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu.

Licha ya Olimpiki kufanyika kila baada ya miaka minne bado Tanzania imekuwa ikishindwa kufanya maandalizi ya kutosha ya kuwaandaa wanamichezo wengi kwenda kushiriki mashindano hayo.

Ukiondoa medali za Nyambui na Bayi, walizoleta mwaka 1980, hakuna mwanamichezo aliyepata mafanikio katika mashindano hayo.

Mara zote tumekuwa tukielezwa sababu ya timu kufanya vibaya katika mashindano makubwa kama Olimpiki ni ukosefu wa maandalizi ya kutosha.

Tunaamini Tanzania ina wanamichezo wengi wenye vipaji, lakini hawaendelezwi na badala yake tunategemea riadha katika mashindano ya kimataifa.

Ni vyema viongozi wa vyama vya michezo wakaiga mfano wa mataifa mengine ya kuziandaa timu zao kwa ajili ya ushiriki wa mashindano ya kimataifa, wasisubiri kutoa sababu zisizokuwa na tija.