MAONI: Vyama vya wakulima virudi kwenye misingi yake

Sunday December 8 2019

 

Dhana ya kuanzishwa kwa vyama vya ushirika vya wakulima, pamoja na mambo mengine ililenga kuwaweka pamoja wakulima na kufanya kazi kwa umoja kama jamii moja.

Ushirika pia huwezesha kupunguza gharama za uzalishaji kama wakulima kuamua kununua pembejeo kwa pamoja .

Kwa kutumia ushirika, wakulima wanajenga nguvu ya pamoja katika kujadili bei ya soko la mazao yao na masuala mengine ya pamoja ya shughuli zao.

Mifumo holela ya ununuzi na kuminywa kwa soko la mazao, ni mwanya unaotunmiwa na wafanyabiashara kunyonya nguvu za wakulima. Wapo walioacha shughuli za kilimo kwa sababu ya dhuluma hii.

Kuwapo kwa vyama vya ushirika vya wakulima kunalenga kuwaondolea adha na unyayasaji huu kutoka kwa wafanyabiashara, madalali na wengineo wasio na nia njema.

Haya ni baadhi tu ya manufaa ya vyombo hivi ambavyo kimsingi vina histioria ndefu nchini kwetu.

Advertisement

Hata hivyo, kadri siku zinavyokwenda, vyama hivi vinazidi kuwatumbukiza wakulima shimoni badala ya kuwanusuru.

Ni lini angalau vitakuwa na sura kama ya vyama vile vya miaka ya sitini na sabini wakati ushirika ulipokuwa na nguvu za kiuchumi na hata upande wa siasa?

Tuna mifano ya shule za sekondari kama vile Omumwani iliyojengwa kwa nguvu ya wakulima wa kahawa kwa kutumia ushirika wa mkoani Kagera. Huu ni mfano mmoja wa vitega uchumi vingi katika maeneo mbalimbali nchini vilivyotokana na uwekezaji uliofanywa na vyama vya wakulima.

Aidha, kupitia vyama hivi ndipo walipoibuka watu maarufu kama George Kahama ambaye alisomeshwa na ushirika hadi ngazi ya chuo kikuu.

Huyu alikuja kuwa mwanasiasa maarufu aliyeshika nyadhifa kadhaa serikalini zikiwamo za uwaziri.

Leo vyama vingi vya wakulima havionekani kuwa na watu wenye maono ya mbali wala dhamira ya dhati ya kuwasaidia wakulima. Vimekuwa uchochoro unaotumiwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi

Ni kwa sababu hii tunaunga mkono jitihada za dhati za Serikali kwa kutoa kauli za kuvibana vyama visivyowajibika, lakini wamekuwa wakivifuatilia utendaji kazi wao na sasa tumeanza kuona matunda.

Tayari baadhi ya vyama ambavyo watendaji wake walituhumiwa kukwapua fedha za wakulima, vimeanza kuzirejesha.

Mfano mzuri ni taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kupokea Sh955 milioni walizopokwa wakulima wa ufuta na vyama vya ushirika.

Tunasifu jitihada hizi kwa kuwa nasi tunahitaji kuona ushirika ukirudi kwenye misingi na maadili yaliyowekwa na waasisi wake.

Tunatoa wito kwa Serikali na mamlaka zake, kama Wizara ya Kilimo, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na vyombo vingine, kuendeleza jitihada ili wakulima wasiendelee kukata tamaa wanaposikia neno ushirika kama ilivyo sasa. Vyama visimamiwe ipasavyo ili hatimaye visaidie katika harakati za ukuzaji wa sekta ya kilimo kama mhimili muhimu katika safari yetu ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda.