UCHAMBUZI: Wachezaji wetu watumie vema mapumziko ya corona kujifua

Serikali imesimamisha michezo yote kwa siku 30 kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, vinavyoenea kwa kasi katika nchi nyingi duniani.

Idadi kubwa ya nchi zikiwamo za Ulaya na Amerika zimesitisha michezo yote na nyingine zimesogeza mbele mashindano hadi Aprili 3 na 4.

Hapa nchini Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa tamko la kusimamisha michezo yote ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi hivyo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu za soka zimeitikia kwa mtazamo chanya agizo la Serikali na tayari zimewapa mapumziko wachezaji.

Idadi kubwa ya klabu zimewataka wachezaji wake kujikinga kwa namna yoyote na maambukizi ya virusi vya corona watakapokuwa nyumbani.

Aidha makocha wa timu hizo wamewataka wachezaji kuzingatia nidhamu watakapokuwa nje ya maeneo ya kazi (kambini) kwa kufanya mazoezi binafsi ili kujiweka fiti.

Kauli za makocha hao ni sahihi kwani kila mchezaji anatakiwa kujitunza ili atakaporejea uwanjani baada ya mashindano kuanza awe fiti kwa ajili ya ushindani.

Kama wachezaji na wanamichezo wengine Ulaya ambao tunawaona katika mitandao wakijifua, vivyo hivyo wanasoka wetu wanatakiwa kufuata nyayo hizo wakiwa katika mapumziko hayo.

Ni fursa nzuri kwao kutumia kipindi hiki cha mapumziko kupumzisha mwili na kujiweka fiti kabla ya kuanza kwa mashindano.

Bila shaka hii ni nafasi nzuri kwao kujiweka sawa kimwili na kiakili baada ya mikikimikiki ya miezi mitatu ambayo kimsingi mwili unakuwa umechoka na unahitaji kupumzika.

Itakumbukwa kwamba kuanzia Januari wachezaji walikuwa na mikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Daraja la Kwanza, Daraja la Pili na Kombe la Azam.

Katika mashindano hayo lipo kundi kubwa la wachezaji wanaocheza mechi mfululizo wakitumika katika kikosi cha kwanza, hivyo watakuwa wamechoka.

Wachezaji wa timu za Ligi Kuu walikuwa na muda mchache wa kupumzika na hata kuimarika baada ya kupata majeraha, kutokana na ratiba ngumu ya kucheza idadi kubwa ya mechi ndani ya muda mfupi kuanzia Januari hadi sasa.

Pia ratiba hiyo ilihusisha safari za mara kwa mara kwa kutumia usafiri wa barabara kutoka mkoa mmoja hadi mwingine.

Kwa wastani kuanzia Januari Mosi hadi sasa, idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu zimecheza michezo 18 katika siku 79, hivyo tofauti ya muda kutoka mechi moja hadi nyingine ni siku nne.

Ndani ya siku hizo nne, baadhi ya timu husafiri kutoka kituo kimoja kwenda kingine, kupumzisha miili baada ya mechi iliyopita na kufanya mazoezi ya kujiandaa na mechi inayofuata.

Lakini kwa timu nyingine, ndani ya kipindi hicho zimekuwa zikikabiliwa na wachezaji wenye majeraha ambao wanahitaji kupona katika muda mwafaka kama huu.

Pamoja na nia njema ya Serikali, wachezaji wetu wasichukulie nafasi hii kama fursa kwao kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili ya mwanamichezo.

Mchezaji anatakiwa kujitunza kwa kufuata miiko ikiwemo kujiepusha na ulevi au starehe ambazo zinaweza kuufanya mwili wake uchoke haraka na hivyo kujiweka katika hatari ya kuumia mara kwa mara wakati mashindano yatakapoanza.

Ili kulinda viwango vyao, nyota hao wa timu mbalimbali wameshauriwa kukitumia kipindi hiki kufanya mazoezi binafsi na pia kujiweka sawa jambo ambalo linaweza kuwapa unafuu makocha pindi wakirejea kambini.

Mbali na hilo, umakini katika matumizi ya vyakula na taratibu nyingine za kiafya unapaswa kuzingatiwa na wanasoka walio mapumzikoni ili kutojiweka katika uwezekano wa kupata majeraha au kuongezeka uzito jambo linaloweza kuathiri programu na mipango ya makocha wao.

Ni kama ambavyo mastaa wa timu zinazoshiriki ligi Ulaya wamekuwa wakitumia kipindi hiki kujiimarisha kwa kufanya mazoezi binafsi katika makazi yao ili kuhakikisha wanalinda ufiti wa mwili.

Mfano wa wachezaji nyota ambao wameonekana kupitia mitandao wakitumia kipindi hiki kujiweka fiti ni beki wa Real Madrid, Sergio Ramos.

Mbali na Ramos, lipo kundi kubwa la wachezaji Ulaya ambao nao wameweka video zao zikiwaonyesha wakifanya mazoezi binafsi katika maeneo mbalimbali gym, ufukweni na wengine nyumbani.

Kama wanavyofanya kina Ramos, wachezaji wetu wana wajibu wa kufuata utaratibu huo ambao utakuwa na manufaa kwao katika kulinda vipaji vyao na manufaa ya klabu.