UCHAMBUZI: Wafanyabiashara mtandaoni acheni ubabaishaji

Mitandao ya kijamii imekuja na fursa nyingi katika maisha ya binadamu. Ni muhimu kwa wajasiriamali wanaochipukia kwa kuwa ni mojawapo ya nyenzo za masoko.

Kutokana na mapinduzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), simu za kiganjani ni muhimu katika kurahisisha shughuli hiyo.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamewafanya wajasiriamali kubuni mbinu za kufanya biashara mtandaoni.

Biashara kwa njia hiyo inaonekana kuwa chaguo la wajasiriamali wengi hasa vijana.

Huenda njia hii inapendwa na wengi licha ya kwamba inaendana na wakati, lakini inawezekana ikawa na unafuu hasa katika kutangaza bidhaa kwa kuwa haihitaji uwekezaji mkubwa.

Mathalani, katika biashara hiyo ya mitandaoni kinachohitajika ni simu “smartphone” au kompyuta yenye kuunganishwa na mtandao wa intaneti pamoja na akaunti ya mitandao ya kijamii au kuwa na tovuti.

Ukiwa na vitu hivyo na bando kwenye simu ya ‘smartphone’ unaweza kuwafikia wateja wengi kwa wakati moja ukizingatia kumekuwa na ongezeko la watumiaji wengi wa intaneti kila kukicha.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Desemba 2017; imeonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imefikia watu milioni 23.

Matumizi haya ya intaneti yamepanua wigo wa biashara, siyo ndani ya nchi tu, bali kimataifa.

Mitandao kama Facebook, Twitter, WhatsApp, Youtube, Instagram na Telegram hivi sasa imekuwa chaguo la wengi ikiwasaidia kutangaza bidhaa na kuwafikia wateja kwa urahisi.

Kupitia mitandao hiyo, vijana wengi wajasiriamali wanaweka picha za bidhaa ikielekeza bei na mahali inakopatikana.

Mathalani, kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp, mjasiriamali anaweza kuposti bidhaa nyingi kwenye ‘status’ ikiambatana na maelezo ya ziada yakibainisha bei ya bidhaa na mahali bidhaa inapopatikana.

Njia hizi za matangazo zinaonekana kuwapa ahueni wajasiriamali kutokana na ukweli kwamba, kutangaza bidhaa kupitia vyombo vya habari kama televisheni, redio na magazeti ni gharama kubwa.

Naiona biashara ya mtandaoni ikiwa mkombozi kwa wajasiriamali hasa kwa kipindi hiki ambacho vijana wengi wanahitimu katika ngazi mbalimbali za vyuo na kuhangaika mtaani bila ajira.

Pamoja na kwamba biashara hii inashamiri, nawiwa kuwakumbusha wajasiriamali hawa kuwa kitu muhimu katika biashara ni uhalisia katika matangazo yao ili kuwaridhisha wateja, hakuna sababu ya kumdanganya mteja kwa kuweka picha za bidhaa ambazo mteja akizihitaji unashindwa kumtimizia.

Nalisema hili kutokana na ukweli kwamba, wafanyabiashara wengi wa mitandaoni wamekuwa na tabia ya kutangaza bidhaa ambazo mteja akizihitaji wanashindwa kumpatia kwa kuwa hawana bali wameziweka kwa ajili ya kuwavutia wateja.

Huu ni udhaifu unaojitokeza kwa wengi waliokimbilia soko la mtandaoni. Kwa namna nyingine, huu naweza nikauita ulaghai.

Unaweka picha zinazoonyesha bidhaa nzuri lakini mteja akihitaji unamzungusha mpaka anakata tamaa.

Nakumbuka miezi kadhaa, nilipitia “status” ya WhatsApp ya mmoja wa marafiki zangu waliojikita kwenye soko la mitandaoni, nikaona ameposti mashati mengi na nikapenda moja, nikamuulizia bei na nikaliagiza baada ya kuridhika na bei.

Ilipita wiki moja bila mafanikio na kila nikimuulizia ananijibu kuwa anatafuta, baada ya wiki moja nilikata tamaa na sikuendelea kumuulizia tena.

Yawezekana hao ni mfano ambao kiuhalisia umeakisi uhalisia wa wafanyabiashara wengi wa mitandaoni na huenda wananchi wengi wanakutana na huo ubabaishaji.

Simaanishi kuwa wote wanaofanya biashara mitandaoni wana tabia zinazofanana, wapo wanaotangaza vitu ambavyo wanauwezo wa kuvimudu kumpatia mteja atakapohitaji.

Ndiyo maana nimeandika makala haya, kuwaangazia wale ambao wanachokitangaza ni tofauti na kile walichonacho nikiamini kuwa, unapomtangazia mteja ni mkataba kuwa utamtimizia pale atakapohitaji kununua.

Unaposhindwa kumuuzia kile ulichotangaza unamkatisha tamaa.

Rai yangu kwa wajasiriamali ambao wameamua kutumia fursa ya soko la mitandaoni, kuweni wakali kwa kuposti vitu ambavyo mnauwezo wa kumpa mteja pale anapohitaji, hii itawajengea uaminifu kwa wateja ikiwa ni njia mojawapo ya kukuza biashara.

Ninachoamini, ukimpa mteja kile anachohitaji, huwezi kumpoteza na pengine anaweza kuwa daraja kukuunganisha na wateja wengine.

Kikubwa ni kuwa uaminifu kwa wateja wa kutangaza bidhaa ambazo una uhakika wa kuwapa wateja wanapozitaka, kinyume na hapo naona ukiwapoteza wateja na hali hii ikijitokeza ni dalili tosha kuwa biashara yako inaenda kufa.

Uchambuzi huu umeandikwa na mwandishi wa gazeti hili anayepatikana kwa simu namba; 0753-590823