UCHAMBUZI: Wanasiasa na siasa zenu za ‘ukinyonga’ mnatuchosha

Ninapoamka asubuhi siachi kusikia siasa za wanasiasa wa ovyo masikioni.

Mara utasikia wabunge wa chama fulani wanunuliwa au mwasisasa mmoja wa chama kile amehamia chama hiki.

Au utasikia kada wa chama hiki amemrushia mishale kada wa chama kile. Chama hiki kimemtimua uanachama kada wao.

Siasa hizi huwa zinaichanganya akili yangu na kushindwa kuelewa kipi ni kipi.

Pengine siyo kwangu tu, lakini inawezekana hali hii ipo pia kwa wananchi wenzangu ambao mara kadhaa wanabaki na mshangao pale wanapoona wale waliowaamini wanakuwa na rangi za kinyonga.

Baadhi ya mambo ambayo hunichanganya zaidi na kunifanya nione siasa kama ‘takataka’ na nisiwe shabiki wa masuala haya ni mitindo ya kuhama hama vyama.

Najua ni haki ya kikatiba kwa kila mtu kuhama au kwenda chama anachokitaka, lakini kwa hiki tunachokishuhudia kwa siasa za nyakati za leo unaweza kusema ni uroho wa madaraka.

Mwaka 2015 kwa waliokuwepo walishuhudia kilichotokea kwa mwanasiasa nguli, Edward Lowassa na wenzake walivyopigwa chini kwenye kura za maoni ndani ya CCM.

Kwa kile alichokiita ‘uamuzi mgumu’ wa kuyasaka mabadiliko, alikuja na upepo mkali uliovuma kwa kasi kiasi cha kushtua wengi na kutimkia Chadema ambako kwa wakati huo ilikuwa imeungana na vyama vingine vya upinzani na kutengeneza umoja ulioitwa Ukawa.

Ndani ya Ukawa mambo yalipamba moto kwa nguli huyu wa siasa ambaye kabla ya kuhamia chama hiki, wafuasi wa Chadema walimuita fisadi na kumtuhumu kuhusika na kashfa kubwa ya Richmond na nyingine kibao.

Wafuasi hawa kupitia viongozi wao akiwamo aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa waliwaaminisha wananchi na kumuona Lowassa si mtu anayefaa hata kidogo.

Walisimama kwenye majukwaa na kuzunguka nchi nzima wakimtaja kwa majina tofauti na tena asiyefaa kuongoza nchi.

Hata hivyo, mara tu baada ya kuhamia Chadema akawa msafi ghafla na wakampa ridhaa ya kugombea urais.

Badala ya kuitwa fisadi tena wakamuita kiongozi wa watu anayejali maskini na anayetaka mabadiliko ya kweli wakisema watamsafisha awe msafi, na ikawa hivyo.

Lowassa akakipuliza kipenga cha kugombea urais akiwa ndani ya Chadema na Ukawa - umoja ambao hapo awali ulitumia nguvu nyingi kumsema kuwa ni fisadi. Wananchi hawakuamini kilichotokea, ni kama walifunikwa na kitambaa cheusi usoni wasione tena yale waliyoaminishwa na wanasiasa hawa.

Wakaanza kumtandikia Lowassa kanga, vitenge na hata kupiga deki lami ili kiongozi huyu apite. Basi mambo yakanoga kwelikweli. Lowassa akawa Lowassa.

Baadhi ya makanda wa Chadema ambao hawakutaka kuona kumuona akikwaa madaraka ambaye sasa amegeuka kiongozi bora akigombea urais kwa tiketi ya chama chao waliamua kujiengua kwenye chama wakidai kimeuzwa.

Pamoja na mbwebwe zote hizo bado mgombea wa CCM, John Magufuli kupitia CCM aliibuka na ushindi mnono. Hapo nguvu ya Lowasasa ikayeyuka tena kama upepo. Akawa kimya kama maji ya mtungini.

Cha kushangaza ni hivi majuzi akaibuka tena na kuwatangazia wananchi kuwa anarudi nyumbani.

Nyumbani ambako awali alikuona hakufai na si rahisi kupatikana mabadiliko ya kweli ambayo aliyatangaza kwa kipindi chake chote cha kampeni na kudai wananchi wasimhoji sana kwa nini anarudi CCM anakokuita nyumbani.

Swali la kujiuliza, ni je Lowassa alifuata nini Chadema na kwa nini amerudi CCM? Waliomnanga wana nini cha kusema na waliomsifu watamnanga tena?

Hayo ni maswali ambayo hayana majibu. Tunabaki kuwa watazamaji na wasikilizaji wa kile kinachofuata katika sinema hii.

Kinachoshangaza zaidi hata wale walioungana naye kuondoka CCM wanatangaza kurudi nyumbani.

Hapo unashindwa kuelewa uhalisia wa usemi wa Mwalimu Julius Nyerere kuwa upinzani wa kweli utatoka CCM.

Wanasisa mnatuchosha. Inafika wakati tunakosa imani nanyi kutokana na tabia zenu za kuwa vigeugeu na matokeo yake ni kusababisha migogoro na makundi ndani ya vyama, jambo linalochangia kudhoofisha vyama hivyo na kukosa dira na hivyo kusababisha visifikie malengo.

Mwandishi anapatikana kwa simu namba 0716-471604