Sido yatoa maeneo ujenzi wa viwanda kanda ya ziwa

Tuesday January 9 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) limekabidhi maeneo yatakayotumika kujenga viwanda vya mfano na ofisi za shirika hilo katika mikoa ya kanda ya ziwa.

Maeneo hayo yametengwa katika mikoa minne ya Simiyu, Mwanza, Geita na Kagera kwa lengo la kuchochea ukuaji uchumi unaotegemea viwanda.

Ujenzi wa viwanda hivyo vinavyotarajiwa kukamilika Aprili utafanywa na Shirika la Suma JKT.

Meneja uendeshaji miradi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanda ya Ziwa, Kapteni Fabian Bubelwa alisema viwanda hivyo vitatumika kutoa mafunzo nchini.

“Tunaanza ujenzi wa viwanda vya mfano mkoani Geita, Simiyu na Kagera. Tutakuwa na ujenzi wa ofisi mbili Geita na Chato, tutajenga mabanda ya viwanda kila eneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo kuongeza thamani ya mazao yao,” alisema Kapteni Bubelwa.

Alisema Kagera zimetengwa eka 4.5 na kwamba ofisi zitatumia eka 1.5 na zitagharimu Sh260 milioni.

Pia, alisema viwanda vya mfano vitagharimu Sh257 milioni.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu alipongeza juhudi hizo zitakazosaidia kuchochea ukuaji uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.

Mkurugenzi mkuu wa Sido, Profesa Sylvester Mpanduji alisema kutakuwa na viwanda vidogo vinne kila mkoa.

“Hili eneo linamilikiwa na Sido kwa miaka mingi. Mkandarasi ametuahidi mwishoni mwa Januari ataanza ujenzi na kutukabidhi ndani ya miezi minne,” alisema.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema viongozi wa mikoa yenye mradi huo wanapaswa kusimamia maendeleo yake na hategemei kuona miradi inazorota na wananchi wanakosa huduma. “Kila mkoa kuna kitu kipya tunachokianzisha na zipo sababu. Kagera tutumie rasilimali zetu zitunufaishe. Tukae na kuzungumza tujue wapi pa kuanzia,” alisema Mwijage.

Advertisement