VIDEO: Jinsi dada alivyomchoma visu mdogo wake hadi kufa

Muktasari:

  • Magreth Reuben aliwasili nyumbani kwake jioni akitegemea kupokewa kwa furaha na mtoto wake wa pekee, Joshua Michael, lakini haikuwa kama alivyotarajia.

Dar es Salaam. Magreth Reuben aliwasili nyumbani kwake jioni akitegemea kupokewa kwa furaha na mtoto wake wa pekee, Joshua Michael, lakini haikuwa kama alivyotarajia.

Badala yake alikuta nyumba ikiwa imetawaliwa na ukimya na barua ya kurasa mbili iliyokuwa juu ya meza.

Barua hiyo ndiyo iliyomfikishia ujumbe kuwa mtoto wa dada yake, Deta Kalambo (19) amemuua Joshua mwenye umri wa miaka miwili.

Kisa hicho kilitokea Jumatatu, wiki hii eneo la Kigamboni Muungano, baada ya Deta aliyekuwa akiishi na mama yake mdogo, Magreth kumuua mdogo wake kwa kumchoma kisu kitovuni kisha kumficha uvunguni mwa kitanda na kukimbilia kwa rafiki yake wa kiume.

Akisimulia jinsi tukio hilo lilivyokuwa, mama wa marehemu, Magreth alisema barua hiyo ya kurasa mbili iliandikwa na Deta baada ya kufanya mauaji hayo.

“Mama naomba unisamehe, umenionya sana ila nimekuwa mkaidi, mimi naondoka naelekea nyumbani,” Magreth alisimulia sehemu ya barua hiyo ilivyoandikwa.

Katika barua hiyo iliyopo katika kituo cha polisi Kigamboni, Deta amemshukuru mama yake Magreth kwa kumlea katika shida na raha, lakini anajutia kosa la kufanya mauaji hayo.

Mama huyo alisema baada ya kusoma sehemu ndogo ya barua alitoka kwenda kwa jirani kumtafuta mtoto wake. “Lakini nikakumbuka kuwa alinitumia ujumbe kuwa mtoto yupo kwa Shafii ambaye ni rafiki yake wa kiume, nikapiga simu polisi,” alisema.

Magreth alishirikiana na majirani kumtafuta mtoto wake kuanzia saa 11 jioni hadi saa saba usiku.

“Nilijaribu kuwasiliana na marafiki na watu wa karibu ili kumpata Shafii ambaye alikuwa na uhusiano na Deta, lakini sikufanikiwa,” alisema.

Baada ya kumsaka kwa siku ya Jumatatu bila mafanikio, Deta alipatikana kwa simu ya mkononi ya Shafii siku iliyofuata akisema mtoto yupo chumbani katika uvungu wa kitanda.

“Nikajiuliza kweli mwanangu tangu juzi (Jumatatu) yuko ndani tu? Mbona akiwa chumbani anaweza kufungua mlango na kutoka nje? Nilishtuka sana, nikamwambia aniletee mwanangu,” alisimuliwa Mama Joshua.

Aliongeza kuwa walipokwenda ndani kama walivyoelekezwa na Deta waliukuta mwili wa Joshua ukiwa umelazwa kifudifudi chini ya uvungu.

Baba wa marehemu, Michael Nzalila alisema hana la kusema kuhusu tukio hilo na kwa wakati huo alisisitiza kuwa anashughulikia mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Sengerema mkoani Mwanza kwa mazishi.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula aliliambia Mwananchi kuwa, walimkamata Deta kwa kutumia namba ya simu ya Shafii.

Alisema baada ya polisi kumpata Shafii anayedaiwa kuwa na uhusiano na Deta walimpigia simu binti huyo kwa kutumia simu ya Shafii.

“Polisi walimpigia simu huyo binti kupitia simu ya huyo mvulana na kumtaka arudi Mikadi Beach, kweli yule binti alikuja na polisi wakamkamata.”alisema.

Kamanda Lukula alisema kwa sasa watuhumiwa wote, Shafii na Deta wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi na watafikishwa mahakamani wakati wowote.