Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhamiaji yataja ugumu uchunguzi wa uraia wa Nondo, Eyakuze

Muktasari:

Baadhi ya watu wanaochunguzwa uraia wao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze; Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe na mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo.

Dar es Salaam. Uchunguzi wa uraia wa baadhi ya watu wanaotiliwa shaka na Idara ya Uhamiaji bado haujakamilika na inaelezwa kwamba ni mgumu na huchukua muda mrefu.

Baadhi ya watu wanaochunguzwa uraia wao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze; Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe na mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo.

Akizungumza na Mwananchi juzi, msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda alisema watu hao bado wanachunguzwa na haijafahamika uchunguzi huo utakamilika lini.

“Uchunguzi wa uraia wa mtu unachukua muda mrefu na hata ukikamilika tunawapelekea majibu wahusika wenyewe. Kwa hiyo siwezi kusema utakamilika lini, kuweni na subira,” alisema Mtanda.

Alipoulizwa kama amerudishiwa hati yake ya kusafiria, Eyakuze alisema haijarudishwa wala hajaambiwa chochote na watendaji wa idara hiyo.

Alisema bado anasubiri kusikia kutoka kwao. “Bado nasubiri kusikia kutoka kwao, passport yangu bado wanaishikilia na hawajaniambia chochote,” alisema.

Eyakuze aliingia matatani Julai ikiwa ni siku chache baada ya taasisi anayoiongoza kupewa barua na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), ikitakiwa kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua kwa kutoa utafiti bila kibali.

Utafiti huo ni ule wa Sauti za Wananchi ulioonyesha umaarufu wa baadhi ya viongozi umeshuka.

Mwingine ambaye yupo matatani ni Askofu Kakobe ambaye wakati wa sherehe za Krismasi mwaka jana alisema kanisani kwake kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali.

Siku chache baadaye kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Charles Kichere alisema kuwa Kakobe hayumo kwenye kumbukumbu za ulipaji kodi wa mamlaka hiyo.

Mwezi Aprili aliitwa na Idara ya Uhamiaji na kuhojiwa kuhusu uraia wake.

Hata hivyo, juhudi za Mwananchi kumpata Askofu Kakobe jana , kuzungumzia hatima ya uchunguzi wake Uhamiaji hazikufanikiwa.

Naye Nondo alihojiwa na maofisa wa Uhamiaji wakati kesi yake ikiendelea Mahakama Kuu. Katika mahojiano hayo, Nondo alitakiwa kupeleka vyeti vya kuzaliwa vya wazazi wake pamoja na vya bibi na babu zake wa pande zote.

Kabla ya kuhojiwa, Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikamatwa na polisi mjini Mafinga, wilayani Mufindi, Iringa na kufikishwa mahakamani akidaiwa kuidanganya polisi kuwa ametekwa.

Akizungumzia suala la Uhamiaji jana, Nondo alisema bado anasubiri uchunguzi ukamilike ili kama atabainika kuwa na hatia afikishwe mahakamani.

“Na wakati nasubiri nimeambiwa nitafute cheti cha kuzaliwa cha bibi na babu mzaa mama au hati zao za kusafiria kwa sababu walisema uthibitisho wa hati za kusafiria upande wa baba pekee niliowasilisha Aprili 20 hazitoshi,” alisema Nondo.