‘Umiliki ardhi wawekezaji uwe miaka 30’

Muktasari:

Wananchi wataka wabanwe, Rais aendelee kuwa mdhamini

Arusha. Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Arusha wamependekeza kupunguzwa ukomo wa umiliki wa ardhi kwa wawekezaji kutoka miaka 90 hadi 30 ili kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi nchini.

Wakitoa maoni kwa kamati inayokusanya maoni ya mabadiliko ya sera ya ardhi ya mwaka 1995, baadhi ya wakazi wa vijiji vya Losinoni na Oldonyosambu wilayani Arumeru, walisema kumpa mwekezaji miaka 90 ni sawa na kumpa ardhi maisha yake yote. Mwenyekiti wa Kijiji cha Losinoni, Joseph Saitobiki alisema ili kuendana na hali halisi ya maisha, wawekezaji wakipewa miaka 30 wataweza kuboresha uhusiano na jamii.

“Wawekezaji wasipewe umiliki wa ardhi wa miaka 99, bali iwe 30 na kama mwekezaji huyo atakuwa mzuri basi anaweza kuongezewa tena miaka 30,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyosambu, Lazaro Laizer, aliunga mkono Rais kuwa mdhamini wa ardhi ya Watanzania pia vijiji kuendelea kuimiliki na kuisimamia.

Laizer alishauri hati za kimila ziwe na nguvu na kuwawezesha wenye nazo kukopa fedha kwenye taasisi za kifedha tofauti na sasa hazitambuliwi na benki.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Oldonyosambu, Samson Ole Sambeke alisema ni vyema Tanzania ikajifunza kutoka nchi za Hispania na Ethiopia zinazotambua ufugaji wa asili. “Tungependa sera hii itambue wafugaji asilia, hawa ni wananchi waliozaliwa eneo fulani na wana haki ya kulimiliki. Wawekewe taratibu ya kumiliki ardhi,” alisema.

Mkazi mwingine, Kalanga Ngoilenga alisema Rais aendelee kuwa na mamlaka juu ya ardhi ili kudhibiti wageni kuja na kuinunua watakavyo kwa kuwa wananchi ndiyo watakaoteseka. Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Kanda ya Kaskazini, Suma Tumpale Mwakasitu, alisema sera ya ardhi ya mwaka 1995 imepitwa na ndiyo maana wanatafuta maoni ya kuwa na sera mpya.