Nec wasisitiza amani

Wananchi wa Kijiji cha Katumba Kata ya Ibighi Wilaya ya Rungwe, Mbeya wakiwa kwenye foleni wakisubiri kupiga kura kwenye Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo. Picha na Godfrey Kahango

Muktasari:

Wapiga kura 333,309 wanatarajiwa kupiga kura leo kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani

Dar ,Mikoani. Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC) imevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika leo Jumapili Novemba 26 unafanyika kwa amani na utulivu.

Akisoma risala kwa umma  jijini Arusha  Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa wapigakura wapatao 333,309 wanatarajiwa kupiga kura.

Amesema uchaguzi huo utakaofanyika katika kata 43 za Tanzania Bara, utakuwa na  vituo 884  ambako ndipo wapigakura wamejiandikishia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.

Juzi Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP), Simon Sirro alisisitiza amani kipindi hiki cha uchaguzi kauli ambayo imeungwa mkono na makamanda wote wa polisi mikoani.

Leo Jumapili asubuhi wananchi wamejitokeza katika kutetea haki zao za kikatiba za kuwachagua viongozi wanaowataka.

"Wananchi wote wasitarajie vurugu zozote na kama zikitokea,wahusika watachukuliwa hatua stahili za kisheria," amesema  IGP Sirro.

Amesema  kwamba jeshi hilo lipo tayari kukabiliana na yeyote atakayejaribu kuvuruga amani na wala halitajali nafasi wala jina la mtu kwenye kuchukua hatua