Uchovu ulivyomlaza Mbowe Muhimbili

 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe 

Dar/Mikoani. Uchovu umetajwa kuwa moja ya sababu zilizomfanya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kupoteza fahamu akiwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana.

Hii ni mara ya pili kwa Mbowe kuugua ghafla na mara moja kupatwa na uchovu uliomfanya kufikia hali ya kupoteza fahamu.

Agosti 2015, mbunge huyo wa Hai aliugua ghafla akiwa katika maandamano ya kumsindikiza aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa baada ya kuchukua fomu ya kugombea katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Machi 5, mwaka huu mwenyekiti huyo alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi baada ya kuugua ghafla alipokuwa akipata chakula na wenzake katika Hoteli ya Keys mjini humo. Katika tukio hilo alilazimika kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua.

Tukio la jana

Mbowe alianguka nyumbani kwake Mikocheni na kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikolazwa kupatiwa matibabu.

Akizungumzia tukio hilo, naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema kinachomsumbua kiongozi huyo ni uchovu kupita kiasi.

“Unajua kwa muda mrefu mwenyekiti amekuwa na shughuli nyingi, lakini wakati huohuo anapaswa kuhudhuria kesi na jana alipata msiba wa kaka yake, hivyo imesababisha afya yake kutetereka,” alisema Mwalimu.

Akizungumza na Mwananchi katika viwanja vya MNH, mkuu wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema Mbowe alianguka saa tisa usiku akiwa nyumbani kwake.

Mrema alisema kabla ya hapo, alikuwa safarini akitokea Dodoma kwa ajili ya kuja Dar es Salaam kusikiliza kesi yake inayoendelea katika Mahakama ya Kisutu.

“Lakini akiwa njiani, alipata taarifa za msiba wa kaka yake Henry Aikaeli Mbowe,” alisema Mrema.

Alisema kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alipofika Dar es Salaam aliendelea na vikao kwa ajili ya taratibu za mazishi.

“Lakini akiwa katika vikao hivyo alikuwa akilalamika kuishiwa nguvu na baada ya muda ndipo alipoanguka saa tisa usiku,” alisema Mrema.

Alisema gari la wagonjwa lilimchukua na kumpeleka Muhimbili na kwamba, hadi jana jioni hali yake ilikuwa inaendelea kuimarika.

“Anaendelea vizuri, nimemuona anaendelea vizuri yupo chini ya uangalizi wa madaktari,” alisema.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Hospitali ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema walimpokea mwanasiasa huyo hospitalini hapo jana saa tisa usiku.

Kesi mahakamani

Wakati Mbowe akilazwa, kesi yake na viongozi wenzake wa Chadema iliendelea kunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wao, Jeremiah Mtobesya aliiambia mahakama hiyo kuwa Mbowe alishindwa kufika mahakamani baada ya kuanguka akiwa nyumbani kwake.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Mtobesya alieleza kuwa Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 112 ya 2018 amefiwa na kaka yake usiku.

Awali wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya Mbowe na wenzake wanane kusomewa maelezo ya awali na upande wa mashtaka wamejiandaa na wako tayari.

Hata hivyo aliiambia mahakama kuwa Juni 12 na 14, 2018 walipokea mapingamizi ya kisheria na wako tayari kuendelea nayo.

Kabla ya kutolewa kwa taarifa hiyo, Wakili Nchimbi aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya Mbowe na wenzake wanane kusomewa maelezo ya awali.

Hata hivyo aliiambia mahakama kuwa mapingamizi ya kesi hiyo yaliyotolewa na mawakili wa Mbowe; Mtobesya na Peter Kibatala yalipokewa na kusikilizwa na mahakama.

Akitoa uamuzi kuhusu mapingamizi hayo, Hakimu Wilbard Mashauri aliyatupiĺia mbali kwa maelezo kuwa wanachokifanya washtakiwa ni kupoteza muda wa kesi hiyo.

Baada ya kutoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 22, 2018 ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali.

Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mwalimu na naibu katibu mkuu Chadema (Bara), John Mnyika.

Wengine ni katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.

Katika mapingamizi yao, mawakili wa utetezi waliiomba mahakama kufuta shtaka la tatu kwa kuwa kuna maneno yameongezwa na hayakuwepo katika hati ya awali ya mashtaka.

Kibatala alidai marekebisho yaliyofanywa katika hati ya mashtaka yameenda zaidi ya amri ya mahakama na kuongeza kuwa, msimamo wa sheria ni lazima amri za mahakama zifuatwe kama ziĺivyo.

Naye Wakili Mtobesya aliiomba mahakama kufuta hati ya mashtaka namba tatu.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alidai kuwa pingamizi la utetezi siyo la kisheria na wakati mahakama inatoa amri haikueleza upande wa mashtaka wakati wakifanya marekebisho nini waongeze na nini wasiongeze.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka tisa ikiwamo kufanya mkusanyiko usio halali na kusababisha vurugu, Februari 16.

Ilidaiwa mahakama hapo kuwa vurugu hizo ndizo zilizosababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

(Imeandikwa na Tausi Mbowe, Tausi Ally na Elizabeth Edward)