Kigwangala aamuru makada wa CCM Tarime kutiwa mbaroni

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla.


Muktasari:

Amri hiyo ilitekelezwa mara moja na askari polisi waliokuwepo kwenye msafara huo.


Tarime. Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Tarime, Newton Mongi na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya chama hicho wilayani humo, Richard Tiboche wanashikiliwa na polisi kwa amri ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla.

Amri ya kukamatwa kwa viongozi na makada hao wa CCM ilitolewa na Waziri huyo jana Julai 16,2018 wakati wa ziara yake ya kukagua maeneo yenye migogoro kati Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) na vijiji vya kata za Nyanungu, Gorong’a na Kwiwamcha wilayani Tarime.

“RPC (Kamanda wa Polisi mkoa) mtie mbaroni huyo kiongozi wa UVCCM kwa kuitukana Serikali. Mkuu wa mkoa mnakaaje na watu kama hawa; mwajiriwa anayelipwa mshahara wa CCM anawezaje kuitukana Serikali ya chama ambacho yeye ni mtumishi wake?” aliamuru Dk Kigwangala na kuongeza:

“Nimemsikia kwa maskio yangu akiitukana Serikali ya CCM ambayo yeye ni kada na kiongozi wake. Kamata na afikishwe mahakamani.”

Amri hiyo ilitekelezwa mara moja na askari polisi waliokuwepo kwenye msafara huo kwa kiongozi huyo kuwekwa chini ya ulinzi huku mwenzake ambaye hakuwepo eneo hilo wakati huo alikamatwa baadaye.

Hata hivyo, hakujulikana mara moja maneno yaliyotamkwa na viongozi hao wa CCM yaliyotafsiriwa na Waziri Kigwangala kama matusi kwa Serikali.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Athuman Mkilindi ambaye yuko kwenye ziara ya Waziri amesema hajui makosa yaliyosababisha amri ya kuwatia mbaroni makada hao wa chama kutolewa na kushauri atafutwe Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe kwa ufafanuzi kwa sababu ndiko makosa yalikotendeka.

Mwananchi lilipomtafuta Mwaibambe alisema makada hao wanashikiliwa na uchunguzi dhidi yao unaendelea.

 “Ndiyo yuko kwenye uchunguzi lakini inadaiwa kuwa alimkashifu Waziri wa Maliasili,” alisema