MSD yasema hakuna mgonjwa atakayekosa ARV's

Muktasari:

  • Mkoa wa Mbeya ni wa tatu kwa maambukizi kitaifa ukiongozwa na Njombe unaoshika nafasi ya kwanza na Iringa nafasi ya pili.

Mbeya.  Pamoja na Mkoa wa Mbeya kuwa na idadi kubwa ya  wagonjwa wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, Bohari ya Dawa (MSD), imesema itahakikisha hakuna anayekosa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi(ARV's).

Mkoa huo ni wa tatu kwa maambukizi kitaifa ukiongozwa na Njombe unaoshika nafasi ya kwanza na Iringa nafasi ya pili.

Akizungumza na waandishi waliopo ziarani mkoani humo, Meneja Kanda ya Mbeya wa Bohari hiyo, Benjamin Hubila, amesema hadi sasa hali ya upatikanaji wa dawa hizo katika vituo wanavyovihudumia ipo vizuri.

Waandishi hao wapo katika ziara ya kujionea utekelezaji wa mpango wa usambazaji wa dawa wa moja kwa moja katika vituo unaofanywa na MSD.

Hubila amesema ingawa kuna uhitaji mkubwa wa dawa hizo ukilinganisha na maeneo mengine wanayoyahudumia, wanahakikisha dawa hizo zinapatikana wakati wote.

“Upatikanaji wa dawa katika maeneo wanayohudumia ikiwemo Rukwa, wilaya ya Makete na Mbeya ni wa asilimia 95 hadi 100,” amesema.

Hubila alizungumzia wizi wa dawa na kusema wanashirikiana na kamati za ulinzi za mkoa na wilaya kufuatilia suala hilo.

"Nadhani suala la wizi wa dawa za serikali pia limepungua kutokana na kuwekwa nembo ambayo ni rahisi kumtambua mtu anayeiiba," amesema meneja huyo.