Acacia yapunguza wafanyakazi tena

Muktasari:

Hili ni punguzo la pili tangu Serikali ilipozuia usafirishaji wa makinikia Machi 2017.

Dar es Salaam. Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia, imepunguza wafanyakazi, kwa kile ilichokiita mabadiliko ya kiutawala.

Pia imetaja sababu nyingine za kupunguza wafanyakazi kuwa ni katika mpango wa kupunguza gharama wakati huu ambapo serikali imezuia usafirishwaji wa mchanga wa madini.

Hii ni mara ya pili kwa Acacia kupunguza wafanyakazi tangu Serikali ilipozuia usafirishaji wa makinikia.  

Serikali ilizuia Acacia kusafirisha makinikia, Machi mwaka jana baada ya agizo la Rais John Magufuli kutaka kuhakikisha serikali inapata mapato ya kutosha katika shughuli za uchimbaji wa madini.

Zuio hilo ambalo mpaka sasa bado halijaondolewa, limesababisha mapato ya kampuni hiyo mwaka 2017 kupungua kwa asilimia 29 ukilinganisha na 2016.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 5, Mkurugenzi wa Acacia, Assa Mwaipopo amesema tangazo la punguzo la wafanyakazi ni la kweli.

“Tangazo ni la kweli, ninashangaa tu umepataje habari hizo wakati liliwekwa kwa ajili ya watu wa ndani tu,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu idadi ya wafanyakazi watakaopunguzwa, Mwaipopo hakutaka kufafanua.

Hata hivyo tangazo hilo limefafanua kuwa upunguzaji huo utafuata taratibu za sheria za kazi na majadiliano baina ya wafanyakazi na uongozi.