Baada ya wanawake, wanaume kuhamia ofisini kwa Makonda

Muktasari:

Makonda alisema wanaume waliolalamikiwa wataitwa na wasipoitikia wito huo majina yao yatatangazwa.

Dar es Salaam. Baada ya mamia ya wanawake wenye watoto ‘waliotelekezwa’ kujitokeza kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, sasa itakuwa zamu ya wanaume kufika ofisini kwa kiongozi huyo.

Wanaume watafika ofisini kwa Makonda kujibu malalamiko ya kutelekeza watoto, huku wenye malalamiko ya kutelekezewa watoto na wake zao nao wakitakiwa kwenda kulalamika.

Akizungumza na wanawake waliofika ofisini kwake jana, Makonda alisema wanaume waliolalamikiwa wataitwa na wasipoitikia wito huo majina yao yatatangazwa hadharani. “Tukikuita hutaki, unajificha na kujidai kulinda ndoa yako wakati mama yangu huku anateseka tutakuanika hadharani mkeo ajue una mtoto nje ya ndoa,” alisema Makonda.

Alisema, “Najua wapo kina baba wasiopenda matokeo yao yaanikwe watanichukia, lakini kunichukia, kunitukana ni kama unanipaka mafuta yanayoning’arisha, chuma kinaimarishwa na moto na viongozi wanaimarishwa na kebehi, kwa hiyo mama zangu msiwe na wasiwasi mmefika sehemu sahihi.”

Makonda aliwataka wanaume waliotelekezewa watoto na wake zao kujitokeza kutoa malalamiko ili wapewe msaada.

Makonda alisema ofisi yake imesheheni wanasheria, wataalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, dawati la jinsia na ustawi wa jamii kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.

Kutokana na wingi wa wanawake waliojitokeza, Makonda alisema uchukuaji malalamiko utafanyika kwa siku tano na ikishindikana zitaongezwa na utawekwa utaratibu ili watu wote wapate huduma.

Makonda pia amezuia magari kuegeshwa nje ya ofisi yake wakati huu wanapoendelea kupokea malalamiko.

Hali halisi ilivyokuwa

Licha ya mvua kubwa kunyesha, wanawake baadhi yao wakiwa na watoto walifika ofisini kwa Makonda maeneo ya Ilala Boma ambako Barabara ya Kawawa ilifungwa kwa takriban dakika 15 alipokuwa akizungumza nao. Waliokosa nafasi kwenye mahema waliloa mvua wakiwa na watoto wao, huku wengine wakisukumana kugombea nafasi ya kutoa malalamiko yao.

“Nipo hapa tangu saa tisa usiku nasubiri kupeleka malalamiko yangu, mwanamume alinitelekeza na watoto watatu miaka miwili sasa, nyumba tuliyopanga nimefukuzwa na sasa watoto wanaishi kwa kuomba mitaani,” alisema Yasinta John, mkazi wa Mbagala.

Alisema wito wa Makonda umempa tumaini jipya kwamba huenda watoto wake wataanza kulelewa na baba yao anayefanya kazi kwenye kampuni moja maarufu jijini Dar es Salaam.

Mwanamke mwingine, Wasra Hana alisema baada ya kujifungua watoto watatu kwa mpigo mumewe alimtelekeza na hajawahi kumpelekea fedha za matumizi.

“Nilishampeleka mume wangu ustawi wa jamii, akaahidi kunipatia Sh60,000 kila mwezi, lakini alitoa miezi miwili na sasa hatoi kabisa,” alisema.

Mwanamke mwingine, Tatu Yusuph aliyefika ofisini kwa Makonda saa tisa usiku (alfajiri) ili kuwahi kuhudumiwa alisema mtoto wake mwenye ulemavu ndiye aliyemsukuma kwenda kumshtaki baba yake.

Alisema mtoto huyo mwenye miaka sita hajawahi kutembea na baba yake alipoona jambo hilo alimtelekeza.

Baadhi ya wanasheria wanaopokea malalamiko hayo walisema idadi kubwa ya wanawake waliojitokeza ni kinyume cha matarajio yao.

“Idadi ni kubwa lakini wanasheria waliopo ni wengi na wataweza kumsikiliza kila mmoja japo si leo (jana). Tunaweza kutumia siku nyingi zaidi,” alisema Moses Basila, mwanasheria kutoka Shule Kuu ya Sheria.

Alisema idadi ya waliojitokeza inaonyesha kuna matatizo ndani ya jamii na njia zilizopo za kuyatatua hazijatoa majibu.

Mwanasheria mwingine, Rehema Mkude alisema wanawake hawapaswi kubaki nyumbani wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia badala yake wakashtaki ili waweze kusikilizwa.

Akizungumzia wito wa Makonda kwa wanawake hao, mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Wanawake (Tamwa), Eda Sanga alisema, “Mimi kama mwanachama mwanzilishi wa Tamwa, tumeshughulikia sana matatizo ya wanawake na kwa kweli nampongeza RC Makonda kwa ubunifu wake. Hiyo ni Dar es Salaam tu, bado matatizo ni makubwa nchi nzima kwa upande wa elimu, afya na jinsia.”

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka alisema Serikali izishirikishe taasisi za dini ili kuziimarisha ndoa kuepusha utelekezwaji wa wanawake.

“Hatua anazochukua Makonda ni nzuri lakini ni dawa ya muda tu. Serikali inapaswa kuzishirikisha taasisi za dini ziimarishe ndoa ili zisivunjike na wanawake kutelekezwa,” alisema Mataka.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mkurugenzi mtendaji wa mfuko wa wanawake Tanzania (WFT), Mary Rusimbi aliyesema mkakati huo utakuwa endelevu ikiwa Serikali itaweka muda wa kutosha wa kusikiliza kero za wanawake.

Rusimbi alisema kujitokeza kwa wanawake wengi ni ishara kuwa tatizo ni kubwa licha ya kuwepo kwa sheria ya ndoa inayosimamia suala hilo.

Akizungumzia ukubwa wa tatizo la utelekezaji wa wanawake na watoto, mkurugenzi wa kituo cha msaada wa sheria kwa wanawake, Tike Mwambipile alisema tatizo ni kubwa hivyo kila mtu ana jukumu la kusuluhisha.

Akieleza uzoefu wake, Waziri wa Mambo ya Ndani wa zamani ambaye ni Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema, “Mimi wakati wangu nilifanya, lakini sikuungwa mkono na Serikali, nikaonekana kama najipendekeza tu kwa wanawake, kumbe nilikuwa nawasaidia waliotelekezwa. Makonda anafanya vizuri, lakini atapingwa hivyo asikate tamaa.”