Babu Tale amchefua Jaji, atakiwa mahakamani J’tatu

Babu Tale


Muktasari:

Babu Tale ambaye ni meneja wa mwanamuziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, alitakiwa kufika mahakamani jana kusikiliza uamuzi wa shauri lake.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa kampuni ya Tip Top Connection, Hamis Shaban Taletale maarufu kama Babu Tale amemchefua Jaji Edson Mkasimongwa wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya kusafiri nje ya nchi bila taarifa na kushindwa kufika mahakamani

Babu Tale ambaye ni meneja wa mwanamuziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, alitakiwa kufika mahakamani jana kusikiliza uamuzi wa shauri lake kuhusiana na uhalali wa amri ya mahakama hiyo kumkamata na kumfunga jela kama mfungwa wa madai.

Hata hivyo hakutokea, badala yake alifika kaka yake Idd Shaban Taletale. Wakili wao, Issa Chondo aliieleza mahakama kuwa Babu Tale hayupo mahakamani kwa kuwa amesafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Kitendo cha kusafiri nje ya nchi bila kutoa taarifa na hivyo kushindwa kufika mahakamani kilimfanya Jaji Mkasimongwa aseme kuwa alichokifanya Babu Tale si cha kiungwana, kauli aliyoirudia mara tatu kuonyesha kuwa kilimuudhi.

Awali Wakili Chondo alidai kuwa mteja wake amekwenda kutibiwa nchini Afrika Kusini, lakini alipobanwa maswali na jaji alijikuta akibadili kauli yake na kusema hajui amekwenda nchi gani, huku akiiomba Mahakama imruhusu awasiliane naye kumuuliza.

Maelezo ya wakili huyo yalimshangaza jaji na kumhoji wakili huyo kuwa inawezekanaje mteja wake ambaye yuko kwenye amri ya kukamatwa asafiri nje ya nchi bila kumuaga wakati anajua kuwa anatakiwa mahakamani.

“Lakini si anajua yuko under arrest? (chini ya amri ya kukamatwa?) Inawezekanaje amekwenda nje ya nchi bila taarifa, sasa huu si uchokozi?” alihoji Jaji Mkasimongwa baada ya Wakili Chondo kutoa taarifa kuwa mteja wake amesafiri nje.

“Kwanza yuko nchi gani?” alihoji tena jaji na wakili huyo akajibu kuwa naye hajajua kuwa amekwenda nchi gani kwani alimtumia tu taarifa, na akaomba Mahakama imruhusu awasiliane naye kumuuliza.

Wakili wa upande wa pili katika shauri hilo, Mwesigwa Muhingo aliingilia kati na kuieleza Mahakama kuwa Babu Tale yuko nchini Marekani na alipotaka kuendelea kutoa maelezo zaidi jaji a alimtaka asubiri kwanza na akaendelea na mahojiano na wakili wa Babu Tale.

“Sasa si huu si ni uchokozi? Kwa nini hajaja kutoa taarifa?” alizidi kuhoji jaji na Wakili Chondo akajibu kuwa alitarajia kuwa angerudi mapema kabla ya siku ya kesi.

“Au mnajua kinachoendelea mahakamani? Wewe wakili wake hujui yuko nchi gani, ina maana na wewe hajakuaga? Au kwa kuwa anajua kesi iko kwa Mkasimongwa ni muungwana, hivyo akakueleza kuwa wewe nenda utamweleza tu hivi.

“Alichokifanya si cha kiungwana, alichokifanya si cha kiungwana, alichokifanya si cha kiungwana. Kwa kuwa kesho nasafiri na narudi Jumapili naamuru tuonane hapa Jumatatu saa 3:00 asubuhi na yeye (Babu Tale) awepo.”

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na naibu msajili, Wilbard Mashauri, Februari 16 iliamuru Babu Tale na nduguye wakamatwe na kupelekwa kifungoni katika Gereza la Ukonga na April 4 akatoa hati ya kuwakamata, kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya mahakama hiyo.

Katika hukumu iliyotolewa na Jaji Augustine Shangwa Februari 18, 2016, iliwaamuru ndugu hao kumlipa fidia ya Sh250 milioni, mhadhiri wa Dini la Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kutokana na makosa ya kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.

Kufuatia amri na hati hiyo Babu Tale alitiwa mbaroni na Polisi Mkoa wa Ilala Mei 22, 2018 na kuhidhiwa kituoni hapo kwa siku mbili akimsubiri Naibu Msajili Mashauri kuidhinisha amri ya kumpeleka gerezani kuwa mfungwa wa madai kwa kuwa hakuwepo.

Lakini Mei 24, Jaji Mkasimongwa akikaimu nafasi ya jaji mfawidhi alimuachia huru kwa muda baada ya kubaini kasoro katika amri ya kuwakamata na kuwafunga.

Mei 25 aliwataka mawakili wa pande zote kutoa hoja zao kuhusu hoja iliyoiibua Mahakama hiyo iwapo msajili ana mamlaka ya kutoa na kusaini amri hiyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote ndipo Jaji Mkasimongwa aliahirisha shauri hilo hadi jana kwa ajili ya kutoa uamuzi iwapo Naibu Msajili Mashauri ana mamlaka ya kisheria kutoa na kusaini amri ya kumkamata na kumfunga mtu aliyeshindwa kutekeleza hukumu ya Mahakama.