Bunge lamaliza utata, Chadema kupeleka wabunge wawili Eala

Muktasari:

Hiyo ina maana kuwa vyama vya ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi vyenye mbunge mmoja kila kimoja vimekosa sifa kutokana na kuwa na uwakilishi mdogo.


Kikao cha Bunge la 11 la Bajeti, kinachoanza kesho kitafunguliwa na hekaheka za uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), ambao tayari Chadema inaonekana kuvuka kikwazo cha kwanza na kujihakikisha nafasi mbili huku CCM ikipata viti sita na CUF nafasi moja.

Hiyo ina maana kuwa vyama vya ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi vyenye mbunge mmoja kila kimoja vimekosa sifa kutokana na kuwa na uwakilishi mdogo.

Uchaguzi huo wa wabunge tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika bunge hilo la Eala umezua mabishano ya kikanuni, huku Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah akitoa ufafanuzi ambao unamaliza malumbano hayo.

Dk Kashililah alisema uchaguzi huo utaendeshwa kwa kutumia Kanuni za Bunge.

“Unaniuliza kuhusu uchaguzi? Soma kanuni, ile ya 12 inaeleza vizuri,” alisema Dk Kashililah.

Kanuni hiyo inaeleza kuwa, “Uchaguzi wa wabunge wanaokwenda katika vyombo vingine ambavyo kwa mujibu wa sheria zilizounda vyombo hivyo vinatakiwa viwe na wawakilishi wa Bunge na uchaguzi wa kuwachagua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki utafanywa kwa kuzingatia, kwa kadri iwezekanavyo, uwiano wa idadi ya wabunge wa vyama mbalimbali vya siasa vinavyowakilishwa.”

Dk Kashililah ambaye ni msimamizi wa uchaguzi huo ametoa ufafanuzi zaidi kwenye taarifa iliyochapishwa katika gazeti la Serikali (GN) la Machi 17 kuonyesha jinsi kila chama kitakavyopata uwakilishi huo.

Katika taarifa hiyo, Dk Kashililah anasema kwa mujibu wa Ibara ya 50 (1) ya Mkataba, Kanuni ya 5(5) na 11(3) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Kudumu za Bunge, na kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania uwakilishi wa wajumbe wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utakuwa katika makundi ya Wanawake, Zanzibar, Upinzani na Tanzania Bara.

“Katika uchaguzi wa mwaka huu mgawanyo wa makundi na upangaji wa idadi ya wagombea katika makundi hayo umezingatia uwiano wa idadi ya wabunge waliopo bungeni kwa kila chama chenye uwakilishi bungeni,” inasema taarifa hiyo ya Dk Kashililah.

Dk Kashililah alitaja uwiano wa idadi ya wabunge kwa kila chama kati ya wabunge 391 waliopo bungeni kwa kufuata vyama kuwa ni CCM yenye wabunge 275 sawa na asilimia 70.33, Chadema yenye wabunge 72 sawa na asilimia18.41, na CUF yenye wabunge 42 sawa na asilimia 10.74.

Kwa upande wa vyama vya NCCR-Mageuzi yenye mbunge mmoja sawa na asilimia 0.25%; na ACT–Wazalendo yenye mbunge mmoja sawa na asilimia 0.25, alisema havitapata wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Kwa kuzingatia uwiano huo, kila chama chenye uwakilishi bungeni kina haki ya kupata viti kwa mchanganuo ufuatao.

Katika taarifa hiyo, Dk Kashililah alisema CCM yenye wabunge 275 sawa na asilimia 70.33 ya wabunge wote inatakiwa kupata viti sita.

Chadema yenye wabunge 72 sawa na asilimia 18.41 ya wabunge wote inatakiwa kupata viti viwili na CUF yenye wabunge 42 sawa na asilimia 10.74 inatakiwa kupata kiti kimoja.

“Chama cha NCCR – Mageuzi na Chama cha ACT-Wazalendo vyenye mbunge mmoja mmoja sawa na asilimia 0.25 havitapata kiti kutokana na kuwa na idadi isiyotosheleza (threshold) kupata nafasi ya uwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki.”

Hivyo kutokana na idadi na uwiano wa wajumbe watakaochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, Dk Kashililah alisema CCM itakuwa na wajumbe Sita, Chadema wawili na CUF mmoja.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Bunge hivi karibuni ilisema uchaguzi huo utafanyika kesho mara baada ya kipindi cha maswali.

CCM yenye wagombea 12 ina nafasi sita na vyama vya upinzani vikiwa na nafasi tatu.

Akitangaza majina hayo hivi karibuni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliwataja walioteuliwa na chama hicho kuwa ni Zainabu Kawawa, Happines Lugiko, Fancy Nkhuhi, Happines Mgalula, Dk Ngwaru Maghembe, Adam Kimbisa, Anamringi Macha na Makongoro Nyerere.

Kutoka Zanzibar ni Maryam Yahya, Rabia Hamid, Abdallah Makame na Mohammed Nuh.

Kwa upande wa Chadema imewateua Ezekiah Wenje na Lawrence Masha ambao kwa mujibu wa kanuni wanaweza kupita moja kwa moja kuwa wabunge.

Chama cha CUF ambacho kwa sasa kimegawanyika katika kambi mbili, kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad kimemteua tena Twaha Taslima kuitetea nafasi hiyo.

Kambi ya Profesa Ibrahim Lipumba imeteua majina matatu ambayo ni Mohammed Habib Mnyaa, Thomas Malima na Sonia Magogo.

Dk Kashililah alisema uchaguzi huo utaendeshwa kwa kutumia Kanuni za Bunge.

Hata hivyo, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alimwandikia barua Spika wa Bunge hivi karibuni, akitaka utaratibu uliotangazwa wa namna ya kupata wabunge ubadilishwe.

ACT Wazalendo imemteua kada wake, Profesa Kitila Mkumbo kuwania nafasi hiyo.

ACT wameshapeleka malalamiko yao kwenye Kamati ya Bunge ya Kanuni wakitaka ibadilishe kanuni hiyo ili nao waruhusiwe kugombea.

Zitto alisema uamuzi wa spika umeacha kuzingatia ukweli wa haki kuwa chama chochote kina haki ya kugombea nafasi yoyote katika makundi yoyote.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema tangazo la Bunge limeweka sharti kwa kila chama kuteua wagombea watatu kwa kila nafasi inayogombewa isipokuwa kwa kundi C.

Zitto alisema ni CCM pekee ndiyo inayolazimishwa na kanuni kuzingatia vigezo vya uwiano wa kijinsia bungeni na pande za Muungano.

Akizungumzia hatua yake ya kugombea ubunge wa Eala, Profesa Kitila alisema mkataba wa Afrika Mashariki haukibani chama chake kusimamisha mgombea.

“Kwanza mkataba wa Afrika Mashariki umeeleza kuwa vyama vyenye uwakilishi bungeni ndivyo vyenye uhalali wa kugombea, pili tangazo la Katibu wa Bunge halijaweka zuio kwa vyama. Halafu uchaguzi huu umekuwa ukifanyika hivyo miaka yote,” alisema Profesa Kitila.

Mwaka 2012 aliyekuwa mgombea wa Eala, Anthony Komu alipinga utaratibu uliokuwa ukitumika katika uchaguzi huo katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).

Komu, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Moshi Vijijini alitaka kanuni ya uwiano wa idadi ya wabunge itumike, alishinda kesi hiyo katika hukumu iliyotolewa Septemba 24, 2014.

Mahakama hiyo ilisema Bunge la Jamhuri ya Muungano lilikiuka kifungu cha 50(1) cha mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki katika uchaguzi wa mwaka 2012.

Hata hivyo, Novemba 2016 Serikali ilishinda katika rufani yake dhidi ya Komu baada ya mahakama hiyo kukiri kuwa haikuwa na uwezo wa kutoa uamuzi huo kwa Bunge la Tanzania ambayo ni mwanachana wa EAC.

Akizungumza na gazeti hili, Jumatatu iliyopita, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema utaratibu wa uwiano umekuwa ukivurugwa kwa miaka mingi hivyo unapaswa kufuatwa.

“Utaratibu wa kupata wabunge wa upinzani wa Eala umevurugwa miaka yote na CCM ili kuwazawadia wanaojifanya wapinzani na kuwaadhibu wapinzani wa kweli,” alisema Lissu na kuongeza:

“Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ndiyo umeunda Bunge hilo unasema wabunge wa Eala watapatikana kutokana na uwiano wa vyama katika mabunge ya nchi wanachama. Uwiano wa vyama pamoja na ‘diversity of opinion (Maoni kinzani)’. Kwa kanuni kuu ni uwiano.”

Alisema uvurugaji huo ulianza kujionyesha mwaka 2005 wakati Chadema ilipokuwa na wabunge 11 lakini nafasi hiyo alipewa Dk Fortunatus Masha aliyekuwa kada wa UDP kilichokuwa na mbunge mmoja. “Kwa hiyo haki ya Chadema ikanyang’anywa kwa sababu UDP walikuwa wanacheza ngoma ya CCM. Ikaja 2010, hakukuwa na Ukawa ila kulikuwa na vita kali kati ya Chadema na CUF na ndiyo tuliwanyang’anya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

“Tulikuwa na viti 49 na tulipaswa kuwa na uwakilishi Eala, badala yake akapewa Nderakindo Kessy wa NCCR Mageuzi ilikuwa na wabunge wanne na baadaye wakawa watano baada ya James Mbatia kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete,” alisema Lissu.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema jana kuwa Kamati ya Kanuni ya Bunge imeyatupa maombi ya ACT kutaka ipewe haki ya kuweka mgombea katika uchaguzi wa Eala.

Bunge la Bajeti

Mbali na uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki, Serikali inatarajiwa kuja na Bajeti mpya ya mwaka wa fedha wa 2017/18.

Akitoa mwelekeo wa Bajeti ya mwaka 2017/18 hivi karibuni Mjini Dodoma, Waziri wa Fedha Dk Philip Mpango alisema Serikali itakusanya na kutumia Sh31.7 trilioni ikilinganishwa na Sh29.5 trilioni ya mwaka 2016/2017.

Alisema fedha zilizotengwa kwa maendeleo zimeongezeka kutoka Sh11.820 trilioni kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ikiwa ni asilimia 40 ya bajeti ya kipindi hicho hadi Sh11.999 trilioni kwa 2017/2018 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.

Hata hivyo, Dk Mpango alisema katika bajeti ya maendeleo, Serikali imeweza kutoa asilimia 34 tu ya fedha za maendeleo jambo lililozua hofu ya utekelezaji wa bajeti mpya.

Dk Mpango alibainisha kuwa washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh3.97 trilioni ambayo ni asilimia 12.6 ya bajeti yote.

Mbali na bajeti, Bunge linatarajiwa kuwa na ugeni wa wabunge waliokuwa gerezani ambao ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Kilomero, Peter Lijualikali.

Lema alikamatwa Novemba 2016 akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli na hakuweza kupata dhamana hadi Machi 2017.

Lijualikali aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miezi sita kwa kufanya vurugu wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015, aliachiliwa Ijumaa iliyopita na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kushinda rufani.

Hata hivyo, Bunge litawakosa wabunge wawili, akiwamo Sofia Simba aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa CCM (UWT), ambaye ni miongoni mwa makada 12 waliofukuzwa kwenye chama hicho.

Mbunge mwingine atakayekosekana ni Dk Elly Macha aliyefariki dunia akiwa nchini Uingereza Ijumaa iliyopita.

Dk Macha aliyekuwa mlemavu wa macho, alifariki akipata matibabu katika hospitali ya New Cross, Wolverhamton, Uingereza.

Wabunge

Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula alisema suala la uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki litazua mjadala mzito kwa sababu ya utata na kutoeleweka kwa kanuni za uchaguzi huo.

“Masuala yatakayoleta mjadala ni yale yaliyoko kwenye ajenda za Bunge. Kwa mfano uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki utazua mjadala kwa sababu ya kutokueleweka kwa tafsiri ya kanuni.

“Tumeona Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akiamwandikia barua Spika kuhusu suala hilo. Kwa hiyo lazima litazua mjadala kama mambo yasipowekwa kwemue misingi ya sheria,” alisema Mabula.

Kuhusu Bajeti, Mabula alisema mjadala utakuwa mkubwa hasa kwa Serikali kueleza utekelezaji wa bajeti iliyopita kabla ya kuanza bajeti mpya.

“Sisi wabunge wa CCM kazi yetu ni kuhakikisha ilani ya uchaguzi inatekelezwa kikamilifu. Kama ile bajeti ya Sh29 trilioni haijatekelezeka, watapata wapi fedha za bajeti ya zaidi ya Sh30 trilioni?

“Kodi zimekusanywa vizuri, lakini bado walipa kodi wachache na kuna kodi nyingi zinazowaumiza walipaji. Kwa mfano, kwenye kodi ya majengo TRA wameshindwa kukusanya. Hakuna halmashauri iliyofikisha asilimia 30 tu,” alisema Mabula.

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul alisema Bunge hili halitakuwa na jipya kwa sababu idadi kubwa ya wabunge ambao ni CCM wametishwa.

“Hoja ni nyepesi tu, hakuna jipya katika Bunge hili, kwa sababu bajeti tunayopanga haitekelezwi na sasa wameleta bajeti ya zaidi ya Sh30 trilioni, yaani ni ‘formalities’ tu,” alisema Gekul.

Aliongeza: “Wabunge wa kuisimamia Serikali wako wapi? Wabunge wa CCM ndiyo wametishwa, si umesikia hadi waliitwa Ikulu? Kwa hiyo watapitisha yale anayotaka Rais tu.”