CAG abaini madudu CWT
Muktasari:
Hayo yamebainishwa katika ripoti ya CAG
Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2016/17 imebaini madudu katika ukaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi ya mwaka 2016/17 leo Jumanne Machi 27, 2018 Ikulu Dar es Salaam ya ukaguzi walioufanya CWT, alisema wamebaini kuna mambo yanayofanywa kinyume cha matakwa ya kanuni za fedha.
“Kwa mfano kulikuwa na malipo yaliyofikia Sh3.5 bilioni ambazo zilifanywa bila kuidhinishwa na Katibu Mkuu na mweka hazina wa CWT kati ya kipindi cha 2011 na 2016,” amesema CAG, Profesa Mussa Assad .
Amesema ukaguzi wa CWT ulifanyika kwa maombi maalumu kwa kuwa siyo sehemu ya mashirika ya umma na baada ya ukaguzi huo ilibaini taasisi hiyo kutoendeshwa sawa sawa.
CAG katika mwaka wa fedha unaoishia Juni, 30 2016 ilibaini kasoro na upungufu katika ukaguzi wa Serikali Kuu, Serikali za mitaa na mashirika ya umma.