CAG afafanua deni la Taifa

Muktasari:

  • Katika makabidhiano hayo, CAG alisema deni la Taifa lililofika Sh46 trilioni kutoka Sh41 trilioni mwaka 2015/16 sawa na ongezeko la asilimia 12, linatia wasiwasi hivyo Serikali inatakiwa kuchukua hatua kupunguza ukubwa huo.

Dodoma. Baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kukabidhi ripoti kwa Rais John Magufuli mwanzoni mwa wiki, ameibuka tena akisema alikosea kutaja takwimu za deni la Taifa.

Katika makabidhiano hayo, CAG alisema deni la Taifa lililofika Sh46 trilioni kutoka Sh41 trilioni mwaka 2015/16 sawa na ongezeko la asilimia 12, linatia wasiwasi hivyo Serikali inatakiwa kuchukua hatua kupunguza ukubwa huo.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Ikulu, CAG alisema: “Ukuaji wa deni ni himilivu lakini jinsi linavyoongezeka, tunakaribia maeneo ya wasiwasi. Asilimia 72 ya GDP (Pato la Taifa) siyo mbaya, lakini ikifika asilimia 76, inabidi tuangalie namna gani tunaweza ku-control (kudhibiti) ukuaji wa deni hilo.”

Licha ya kukosea huko tofauti na taarifa iliyomo kwenye ripoti yake, Rais Magufuli alimtoa wasiwasi akisema nchi inakopa na kuzitumia fedha hizo kutekeleza miradi ya maendeleo.

CAG alikabidhi nakala ya ripoti yake kwa Rais katika tukio lililorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) akisema suala hilo lilipaswa kuwa siri kwa umma hadi itakapowasilishwa bungeni kabla ya Aprili 12 kwenye Bunge la Bajeti.

Baada ya kubaini alichokizungumza mwanzoni mwa wiki kuwa siyo sahihi, jana Profesa Assad alirekebisha kauli yake kuhusu mwenendo wa ukuaji wa deni la Taifa akisema: “Taarifa sahihi kuhusu mwenendo wa deni hadi Juni 30, 2017 lilikuwa Sh46 trilioni. Katika deni hilo, Sh13.34 trilioni sawa na asilimia 29 ni deni la ndani na Sh32.75 trilioni sawa na asilimia 71 ni deni la nje. Deni hilo lote ni sawa na asilimia 31 ya Pato la Taifa ambalo bado ni himilivu.”

Profesa huyo alisisitiza kwamba kilichokosewa ni matamshi yake lakini ripoti nzima iko vizuri na itakuwa wazi kwa ajili ya umma kufahamu kwa kila kitu kilichomo.