Chadema walaani kutekwa mgombea udiwani

Mgombea udiwani wa Kata ya Guhangaza, wilayani Muleba mkoani Kagera, Mchungaji Athanas Kakoti akiwa amelazwa katika Hospitali ya Kagondo jana baada ya kuokotwa barabarani akiwa hajitambui na kupelekwa hospitali na wasamaria wema. Picha na Mpigapicha Maalumu

Muktasari:

Wakati Chadema ikilaani tukio hilo lililotokea Februari 2, aliyekuwa mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Manzase wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Mashaka Chalo amejiunga na CCM pamoja na wanachama wengine 131 wa chama hicho cha upinzani.

Dar/mikoani. Chadema imelaani tukio waliloliita la kutekwa kwa mgombea wake wa udiwani Kata ya Guhangaza wilayani Muleba mkoani Kagera, Mchungaji Athanas Makoti (28) aliyepatikana jana alfajiri akiwa hajitambui.

Wakati Chadema ikilaani tukio hilo lililotokea Februari 2, aliyekuwa mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Manzase wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Mashaka Chalo amejiunga na CCM pamoja na wanachama wengine 131 wa chama hicho cha upinzani.

Wakati Chadema ikisema Makoti alitekwa, polisi juzi ilieleza kuwa taarifa zilizowasilishwa kwao ni kwamba alitoweka baada ya kuondoka nyumbani na kutorejea.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene chama hicho kimelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza tukio la kutoweka Makoti ambaye anatibiwa katika Hospitali ya Kagondo, baada ya kuokotwa kando mwa barabara ya kuelekea Bukoba.

“Tangu Makoti alipotoweka Polisi haikufungua jalada la uchunguzi. Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi makao makuu kuingilia kati ili uchunguzi wa haraka kuhusu suala hilo ufanyike,” alisema Makene.

Chama hicho pia kimeiomba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBU) kutumia mamlaka yake kuhakikisha tukio hilo linafanyiwa uchunguzi wa haraka kuwabaini wahusika na kuchukua hatua.

“Pia tunaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukemea vitendo kama hivyo ambavyo vinatia doa mfumo wa uchaguzi na demokrasia nchini, ukimya wao unaashiria wanakubaliana na tabia hii mpya ya utekaji ambayo tuliilalamikia hata wakati wa uchaguzi wa marudio wa kata 43, Novemba mwaka jana,” alisema Makene.

Akizungumza na Mwananchi jana, katibu wa Chadema wilayani Muleba, Elisha Kabombo alisema Makoti alitelekezwa na watu wasiojulikana jirani na Hospitali ya Kagondo.

Alisema wananchi waliokuwa wakipita eneo hilo usiku wa kuamkia jana walimuona akiwa kando mwa barabara ya kuelekea Bukoba, hivyo kumpeleka hospitali.

“Hali yake si nzuri kwa sababu hawezi kuzungumza vyema wala kuketi. Kawekewa dripu za maji. Tuzidi kumuombea,” alisema.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Isack Msangi alithibitisha kupokea taarifa za kupatikana mgombea huyo. Alisema vyombo vya dola vinamhoji ili kuendelea na uchunguzi.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kagondo, Dk Humphrey Batungi alipoulizwa afya ya mgombea huyo alisema ni mapema kuizungumzia.

Katibu wa uenezi wa Chadema Jimbo la Muleba Kusini na mratibu wa chama hicho Jimbo la Muleba Kaskazini, Hamisi Yusufu alisema baada ya kufikishwa hospitali alikutwa akiwa na majeraha, huku akizungumza kwa shida.

Alisema Makoti aliwaeleza amenyang’anywa fedha, waliomteka walimfunga kitambaa cheusi usoni na kumtaka asigombee uchaguzi utakaofanyika Februari 17 na amekiri kuwafahamu baadhi ya waliomteka.

Mgombea Chadema ahamia CCM

Juzi, katika Kata ya Manzase wilayani Chamwino, naibu katibu mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo alimpokea mgombea udiwani wa Chadema, Chalo alipozindua kampeni za udiwani katika Kijiji cha Manzase.

Chalo amehamia Chadema ikiwa ni siku ya tatu tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuzindua kampeni katika kata hiyo, akinadiwa na mbunge wa viti maalumu, Kunti Majala.

Katika mkutano huo, mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema uamuzi wa Chalo kujiuzulu ni ushindi kwa chama tawala.

“Mpogolo unaweza kufungua kampeni hizi na kisha kuzifunga maana kazi imekwisha. Tulikuwa na wagombea watatu, lakini kuondoka kwa huyu, CCM tunaona kazi imekwisha. Wagombea wengine waliobaki hata tukilala usingizi hakuna kitu ushindi ni wetu,” alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, Chalo alisema amerejea CCM kwa sababu ni chama chake na kimemlea.

Imeandikwa na Shaaban Ndyamukama (Muleba), Burhan Yakubu (Tanga), na Habel Chidawali (Dodoma).