Diamond: Nilitaka mwanangu aitwe Dylan nashangaa kuitwa Abdul

Muktasari:

  • Ameeleza jinsi alivyotaka mtoto wake kwa Mabetto aitwe Dylan

Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond Platnumz amesema jina alilotoa apewe mtoto wake kwa Hamisa Mobetto ni Dylan lakini kwa sababu za kutafuta umaarufu mwanamke huyo alimwita Abdul Nassib.

Amesema Hamisa alimwita mtoto huyo Abdul ambalo ni jina la baba yake mzazi ili iwe rahisi watu kufahamu kuwa mtoto huyo ni wa kwake baada ya kukubaliana kufanya uhusiano wao kuwa wa siri.

“Mimi jina ninalolitambua ni Dylan hata niliposikia wamemwita Abdul nilisema poa tu lakini akija kwangu nitamwita ninalolitaka mimi kwa sababu nataka aitwe DD (D Square).”

Amesema alisikitishwa pia na kitendo cha mwanamke huyo kumualika baba yake katika sherehe ya kutimiza siku arobaini ya mtoto huyo akimdanganya kuwa angekuwepo.

“Walimwalika mzee Abdul na nguo wakampelekea ili ahudhurie, yote hiyo ili mradi tu wapate cha kuzungumziwa mitandaoni,” amesema.