Diamond amkumbatia Wema mashabiki washangilia

Muktasari:

Ni mara kadhaa walionekana wakikumbatiana na wakati mwingine Diamond akichezea nywele za Wema Sepetu ambaye amewahi kuwa mpenzi wake.

 

Dar es Salaa.Mastaa Wema Sepetu na Diamond Platnumz wameibua mjadala upya kutokana na ukaribu waliouonyesha wakati wa hafla ya kumkaribisha mwanamuziki mpya katika lebo ya Wasafi, Mbosso katika ukumbi wa Maisha Basement jijini Dar as Salaam.

Wawili hawa walionekana kuwa pamoja wakitawaliwa na pozi zenye utata hali iliyoulipua ukumbi huo kwa shangwe kutoka kwa mashabiki.

Ni mara kadhaa walionekana wakikumbatiana na wakati mwingine Diamond akichezea nywele za Wema Sepetu ambaye amewahi kuwa mpenzi wake.

Pamoja na mashabiki kushangilia, hakuna hata mmoja kati yao ambaye alionyesha kuwa na wasiwasi kutokana na mambo waliyokuwa wakiyafanya bila kujali kamera zilizokuwa zikiwamulika.

Wema alikuwa miongoni mwa wageni waliopandishwa jukwaani katika hafla hiyo kwa ajili ya kuwasalimu mashabiki.

Alipopanda jukwaani kelele zilizizima kutoka kwa mashabiki wakionyeshwa kufurahia mrembo huyo kwa mara nyingine kupanda kwenye jukwaa la WCB.

Kitendo hicho kimepokelewa kwa mtazamo tofauti katika mitandao ya kijamii hasa Instagram ambao mastaa hao wana mashabiki wengi.

Wapo walioonyesha kufurahishwa na hilo na kuwapongeza huku wakimrushia vijembe mzazi mwenzake Diamond, Zari.Wengine wameonyeshwa kukerwa na kitendo hicho na kumtupia lawama Wema kwa kuruhusu hali hiyo.

Wengi wamelifananisha tukio la jana na kilichowahi kutokea mwaka 2013 kati yao   aliyekuwa mpenzi wa Diamond, mtangazaji Penny.

Wakati Diamond akiwa kwenye uhusiano na Penny baada ya wao kuachana, picha zao zilivuja zikiwaonyesha wakiwa mapumzikoni nje ya nchi.