FCC yabaini tatizo makasha 415 ya bidhaa
Muktasari:
Waziri Mwijage amesema tume ilifanya operesheni saba na kukamata bidhaa zilizokiuka alama za bidhaa.
Dodoma. Makasha 415 kati ya 4,004 yaliyokaguliwa Bandari ya Dar es Salaam na Tume ya Ushindani nchini (FCC), yalibainika kuwa na bidhaa mbalimbali zilizokiuka sheria ya alama za Bidhaa ya Mwaka 1963.
Ukaguzi huo ulifanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha, 2018/19.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha 2018/19, waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage amesema pia FCC ilifanya kaguzi wa kushtukiza katika maduka na maghala jiji la Dar es Salaam.
“Katika kaguzi hizo watuhumiwa 56 walikamatwa na bidhaa bandia zikiwamo vilainishi vya magari, vifaa vya mabomba na kofia ngumu za pikipiki,”amesema.
Pia amesema tume ilifanya operesheni saba na kukamata bidhaa zilizokiuka alama za bidhaa katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro, Mtwara, Shinyanga, Songwe na Tanga.
“Katika operesheni hizo watuhumiwa wapatao 94 waliokamatwa na bidhaa bandia zikiwamo dawa za meno na miswaki, wino, mvinyo, vifaa vya ujenzi, vifaa vya mambo, mabati ya kuezekea, viatu na sabuni,”amesema.
Ametaja bidhaa nyingine zilizokamatwa ni mafuta ya maji ya kupaka, pampu za kumwagilia maji, maji ya tindikali na pikipiki.