Familia ya Lissu yakerwa

Muktasari:

  • Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Simon Sirro, kueleza kuwa dereva huyo anahitajika kusaidia katika uchunguzi ili kuwapata watu waliohusika kumshambulia mbunge huyo.

Dar es Salaam. Familia ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu imelishauri Jeshi la polisi kumfuata dereva wa mbunge huyo ambaye kwa sasa yupo Nairobi kwa ajili ya mahojiano ili kukamilisha upelelezi wao.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Simon Sirro, kueleza kuwa dereva huyo anahitajika kusaidia katika uchunguzi ili kuwapata watu waliohusika kumshambulia mbunge huyo.

Kaka wa Lissu, Alute Mugwai alisema anashangaa hadi sasa kusikia polisi wanazungumza kwenye vyombo vya habari wakimtaka dereva huyo wakati wana uwezo wa kumfikia.

Alisema polisi wana uwezo wa kumfuata dereva huyo Nairobi na kumfanyia mahojiano ili kuruhusu upelelezi huo kuendelea kuliko kuliko kusimamisha shughuli zote wakimsubiri hadi atakaporudi.

“Inawezekana vipi polisi wasimamishe shughuli kwa sababu ya mtu mmoja. Kwa sababu yeye yupo kule kwa ajili ya matibabu na kumuangalia bosi wake , tunashauri wapeleke mpelelezi kule, wamchukue waende naye kwenye ofisi za ubalozi wachukue maelezo yake badala ya kusubiri hadi arudi,”

“Wanaposema hadi arudi huku vipi kuhusu usalama wake, maana hadi sasa hakuna hata mmoja aliyekamatwa kuhusiana na uhalifu huo, anarudije na kwa usalama kiasi gani,” alihoji Mugwai

Alisema, “Tunaamini katika eneo lile kuliko na watu, pale kuna nyumba ya naibu spika lazima ana mlinzi, hii ina m maana kuwa mashahidi walikuwepo wengi sio dereva peke yake. Hao nao wangetumika kusaidia upelelezi kuliko kumsubiri dereva wa Lissu,”.

Kuhusu kama upo uwezekano wa dereva huyo kuhusika katika shambulio hilo Mugwai alisema “Tunachotaka uchunguzi wa kina ufanyike, kama atahojiwa na kukutwa anahusika nina imani atachukuliwa hatua kama wahalifu wengine,”

“Dereva huyu amekuwa na Lissu kwa muda mrefu, ni kama mzazi wake amemlea tangu mdogo wana miaka karibu 25 wakiwa pamoja lazima na yeye atakuwa ameathirika kutokana na tukio hili,” alisema Mugwai

Ushirikiano na serikali

Mugwai alisema kwa kuwa lengo la familia hiyo ni kutaka Lissu anapata matibabu na waliomdhuru wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria hawana sababu ya kukwepa kushirikiana na serikali.

Alisema familia ilikutana na Spika wa bunge, Job Ndugai kwa saa nne kwa lengo la kujadili matibabu ya Lissu na mazungumzo yao hayakumilika na wakakubaliana wataendelea siku nyingine.

“Sisi hatupigi siasa ndiyo sababu tumeamua kushirikiana na serikali na hatuko tayari kuona suala hili linaendeshwa kisiasa lengo letu apone na ukweli ujulikane, hali ya Lissu isitumike kufanya siasa. Tunataka utaratibu wa kawaida ufuatwe bila kuingiza siasa,”

Alisema tayari familia imeshaandika barua kwa serikali kuomba uchunguzi ufanyike kwa kina, haraka na kitaalam ufanyike kuwabaini waliohusika na kutaka ushiriki wa wapelelezi wa nje kuharakisha uchunguzi huo.

“Tumekuwa na kikao na mwanasheria mkuu, tumeona pia waziri wa sheria na katiba, wameelewa maombi yetu na wamesema watayafanyia kazi, na kwa kuwa lengo ni jema basi waruhusiwe wapelelezi wa nje. Tunaona hakuna ‘seriousness’ katika kupata ukweli wa suala hili,”

Hali ya Lissu

Mugwai alisema hali ya mbunge huyo inazidi kuimarika na sasa ameanza kuongea na kula kwa njia ya kawaida.

“Lissu anaimarika, amefanyiwa upasuaji mara kwa mara. Ameanza kula kwa njia ya kawaida na kuzungumza vizuri, ndugu yetu aliyeenda kule juzi ametupa taarifa hizo jana kuwa afya yake inazidi kuimarika”

Zuio la maombi

Kaka mwingine wa Lissu, Vicent Mugwai alisema anashangazwa na kitendo cha kuwazuia watu wanaokusanyika kumuombea ndugu yake kwa kuwa hakuna kosa wanalolifanya.

“Vitendo vya kuwazuia watu kuvaa tisheti zilizoandikwa ‘Pray for Lissu’ na kukusanyika kumuombea vinatia shaka. Kwanini uwazuie watu kumuombe mtu aliyeumizwa ili apone? Tunawashukuru watanzania wanaoendelea kumuombea na tuna imani maombi yao yanamsaidia Lissu,”

Kuhusu kutokamatwa kwa mtu yeyote hadi sasa Vicent, “Hii inaanza kutupa shaka unakaribia kuisha mwezi sasa hakuna aliyekamatwa, wakati siku zilizofuata kuna askari alipigwa risasi na wahusika wakapatikana”

“Ikumbukwe kuwa Lissu alishasema kuna watu waliokuwa wanamfuatilia na alitaja hadi namba za gari, sisi tulitegemea hao ndio wangeanza nao kwenye upelelezi,” alisema Vicent