Hatima ya kuzikwa mwili wa Kapange kujulikana siku ya 160 akiwa mochwari

Muktasari:

Frank alifariki dunia Juni 4 katika tukio ambalo liligubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba Soko la Sido jijini Mbeya, alifariki dunia kwa kipigo akiwa mikononi mwa Polisi, hivyo kususia mwili huo ambao hadi sasa upo chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ikiwa ni siku ya 157.

Mbeya. Mwili wa Frank Kapange (21) utaendelea kukaa mochwari ya Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa zaidi ya siku 160 ukisubiri uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya utakaotolewa Novemba 12.

Uamuzi huo utahusu hatima ya rufaa ya kesi iliyofunguliwa na familia ya Kapange dhidi ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya wa kutupilia mbali maombi yao ya kutaka mwili wa kijana huyo ufanyiwe uchunguzi kabla ya kuzikwa.

Frank alifariki Juni 4 na kifo chake kiligubikwa na utata kiasi cha ndugu zake kugoma kuuchukua mwili kwa ajili ya maziko. Mwili huo leo unatimiza siku ya 155 na hadi uamuzi huo utakapotolewa Novemba 12, utakuwa umefikisha siku 161.

Gharama za kuuhifadhi mwili huo kwa siku ni Sh20,000 hivyo hadi Novemba 12, itakuwa imefikia Sh3.22 milioni.

Agosti 24, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite aliamuru mwili wa Frank kuchukuliwa na ndugu ili ukazikwe baada ya kutupilia mbali maombi ya familia ya kuiomba mahakama hiyo iamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kiini cha kifo chake baada ya kuridhika na mapingamizi yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa Serikali.

Hata hivyo, ndugu hao hawakuridhishwa na uamuzi huo hivyo wakaamua kukataa rufaa Mahakama kuu Kanda ya Mbeya.

Jana, akitoa hoja za kukataa rufaa hiyo na kuishawishi mahakama hiyo kutengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya wa kuifuta kesi hiyo, Wakili wa utetezi, Moris Mwamwenda alidai hakimu aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kutupilia mbali shauri hilo.

Pia, alisema walipeleka maombi ya kesi ya jinai namba 2 ya mwaka 2018 lakini hakimu aliyetoa uamuzi aliandikia uamuzi mdogo wakati kesi ya msingi haikusikilizwa.

“Maombi ya msingi hayakusikilizwa, hivyo hapakuwa na uhalali wowote kutupilia mbali shauri hili kwa hoja za mapingamizi ya awali,” alisema Wakili Mwamwenda.

Pia, Wakili huyo alisema sababu nyingine, wanapinga amri iliyotolewa na mahakama ya kumuamuru Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, kuutoa mwili huo na kuwakabidhi ndugu na kama watakaidi uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na uongozi wa Jiji la Mbeya wabebe jukumu la kwenda kuuzika mwili huo.

Wakili huyo alisema kutokana na hoja hizo, wanaoimba Mahakama Kuu kutengua uamuzi huo na kuamuru kesi hiyo kurudi katika mahakama hiyo (Hakimu Mkazi-Mbeya) kwa ajili ya kuanza kusikiliza upya.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na wakili wa Serikali, Baraka Mgaya ambaye alidai mapingamizi yao ya awali yalikuwa ya kisheria ndiyo maana hakimu aliyakubali.

Mgaya alidai kiapo chochote lazima kiwepo katika shauri husika na kisainiwe na mtu sahihi kisheria na kionyeshe mahali kilipotolewa na kama kiapo hicho hakitakuwa na vitu hivyo, kitakuwa kimekosa uhalali wa kisheria.

Wakili Mgaya alidai mkata rufaa, hakupaswa kukataa rufaa Mahakama Kuu, bali angerudi kwenye mahakama iliyotoa uamuzi wa kutupilia mbali maombi yao kwa ajili ya kuishawishi itengue uamuzi wake ili itoe uamuzi wa pande zote mbili kwa vile awali ilitoa uamuzi wa pande mmoja.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji anayesikiliza rufaa hiyo, Paul Ngwembe alisema atatoa uamuzi wake Novemba 12 na kufanya hivyo kutokana na asili ya kesi yenyewe inavyovuta hisia katika jamii.