Huduma ya usafiri kisiwa cha Ukara kuanza kesho

Wataalam wa uokoaji wakiendelea na kazi ya kukinyanyua kivuko cha Mv Nyerere.

Muktasari:

Wakati operesheni ya uokoaji na kazi ya kukinyanyua kivuko cha Mv Nyerere ikiendelea, Serikali imeagiza kivuko cha Mv Temesa chenye uwezo wa kubeba abiria 120 kianze kutoa huduma ya usafiri kati ya kisiwa cha Ukara na Kisiwa Kikuu cha Ukerewe eneo la Bugorola kuanzia kesho Septemba 26


Ukara. Huduma ya kusafirisha kwa abiria na mizigo kutoka na kwenda kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe jijini Mwanza itarejea katika hali ya kawaida kuanzia kesho Septemba 26,2018.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isaac Kamwelwe amesema leo Septemba 24,2018 kwamba huduma hiyo itatolewa kupitia kivuko cha Mv Temesa.

"Serikali inatekeleza mipango mahususi ya dharura kuhakikisha wakazi wa kisiwa cha Ukara wanapata huduma ya usafiri kwa kuagiza mafundi kukifanyia uchunguzi wa kitaalam kivuko cha Mv Temesa na kukileta Ukara kitoe huduma. Usafi kati ya Ukara na Bugolora utarejea Jumatano (kesho Septemba 25)," amesema Waziri Kamwelwe

Amesema kivuko hicho cha Mv Temesa chenye uwezo wa kubeba abiria 120 kitatoa huduma hadi hapo ujenzi wa meli mpya ya tani 50 ambayo Rais John Magufuli ameagiza tenda yake itangazwe utakapokamilika.

Tangu Septemba 20, 2018 kivuko cha Mv Nyerere kilipopinduka, wananchi wanaosafiri kati ya kisiwa cha Ukara na Bugolora wanategemea meli binafsi ya Mv Nyehunge inayotumika kusafirisha vifaa, zana, magari, mitambo, wataalam, Maofisa na viongozi mbalimbali wanaofika Ukara kutoa pole, kukagua au kushiriki operesheni ya uokoaji.

Meli hiyo pia ndio hutumika kusafirisha miili ya waliokufa katika ajali hiyo inayochukuliwa na ndugu kwa mazishi nje ya kisiwa cha Ukara.

Hadi kufikia jana jioni ya Septemba 24,2018 miili ya watu 226 waliokufa katika ajali hiyo ilikuwa imeopolewa huku watu 41 wakiokolewa wakiwa hai akiwemo fundi Mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere, Alphonse Charahari aliyeokolewa karibia saa 48 tangu kivuko kilipopinduka.

Soma zaidi: