JKCI yawezeshwa operesheni ya watoto 138

Mkurugenzi mtendaji wa  I & M Bank, Basser Mohamed akimkabidhi zawadi, Elizabeth  Magau jana ambaye ni mmoja kati ya watoto 150 wanaosubiri kufanyiwa upasuaji  wa moyo katika   Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Dar es Salaam kwa msaada wa taasisi mbalimbali.  .  Picha Omar Fungoo .Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Wakati fedha hizo zikitolewa, JKCI inahitaji takriban Sh800 milioni ili kukamilisha upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto 500 wanaohudhuria kliniki na ambao wameshaidhinishwa kwamba wanahitaji matibabu hayo.

Dar es Salaam. Watoto 138 wenye matatizo ya moyo wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji mwezi ujao, baada ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kukabidhiwa msaada wa Sh303 milioni kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.

Wakati fedha hizo zikitolewa, JKCI inahitaji takriban Sh800 milioni ili kukamilisha upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto 500 wanaohudhuria kliniki na ambao wameshaidhinishwa kwamba wanahitaji matibabu hayo.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo jana, Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi alisema fedha hizo zitawezesha upasuaji kwa watoto hao waliotakiwa kufanyiwa mwakani. Pia, amewaomba wahisani kutoa msaada zaidi.

Alisema fedha hizo ziliwasilishwa na taasisi tatu za Baps Charities iliyotoa Sh222 milioni, Youth Welfare Trust (Sh48.4 milioni) na I & M Bank (Sh33 milioni).

“JKCI tunatoa shukrani kwa taasisi hizi. Mwaka huu tumeshafanya upasuaji kwa watoto 234, hata wenzetu wanaotusaidia wanaona fedha zinavyotumika na kati ya hao, watoto 100 walifanyiwa kwa msaada wa Baps Charities.

“Tunawaahidi kabla ya katikati ya mwezi ujao tutakuwa tumekamilisha upasuaji kwa nusu yao, tunaamini itatusaidia kuokoa watoto wengi. Tunaomba wengine wajitokeze kwa sababu wanaohitaji huduma ni wengi na watoto bado wanazaliwa wakiwa na tatizo la moyo,” alisema.

Profesa Janabi alisema wameanzisha uchunguzi mpya kwa wajawazito na kati ya 27 waliopimwa, watoto watatu wamegundulika kwamba watazaliwa wakiwa na tatizo la moyo.

“Juhudi mbalimbali zinaendelea ili kuhakikisha tunapunguza tatizo hili,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank, Baseer Mohammed alisema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya Watanzania ambao awali hawakuwa na uwezo wa kwenda nje ya nchi kwa matibabu.

“Tumetoa kwa ajili ya jamii, fedha hizi ni kidogo lakini tuna imani zitasaidia watoto 15 kupata huduma ya upasuaji,” alisema Mohammed.

Katibu wa Baps Charities, Paresh Chollera alimshukuru Profesa Janabi kwa kutoa huduma nzuri kwa awamu ya kwanza ya msaada huo.

“Januari, tulitoa Sh222 milioni na watoto 100 walifanyiwa upasuaji kwa mafanikio makubwa, hili limetutia moyo na tukahamasisha wengine kuchangia, sasa tumewasilisha kiasi hicho kwa mara nyingine ili watoto 101 wapatiwe matibabu,” alisema Chollera.

 

Sh800 milioni zahitajika

Mkurugenzi wa Utafiti wa JKCI, Dk Pedro Palangyo alisema bado taasisi hiyo inahitaji fedha nyingi zaidi ili kukamilisha upasuaji kwa wenye mahitaji.

“Tuna wagonjwa 500 wanaohitaji kufanyiwa upasuaji, kwa hiyo fedha hizi zitahudumia sehemu ndogo ya hawa; bado mahitaji ni makubwa zaidi, kwa wagonjwa hao. Zinahitajika si chini ya Sh800 milioni,” alisema.

Dk Palangyo alisema mwaka jana taasisi ilifanya upasuaji wa kufungua vifua na kwa njia ya mtambo maalumu wa Cathlab. Alisema walihudumia wagonjwa 224 na mwaka huu wamefikia 494 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 200.

“Kwa upande wa upasuaji, mwaka jana tulihudumia wagonjwa 204 na mwaka huu tumewafikia 234, hii ni sawa na ongezeko la asilimia 109. Kwa jumla tumetoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa 728 kwa miaka miwili,” alisema Dk Palangyo.