JPM kutoa Sh1milioni kila mfiwa, majeruhi MV Nyerere

Muktasari:

  • Uamuzi huo wa Rais umetangazwa leo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe na fedha hizo zitatolewa kwa wafiwa wote na walionusurika katika ajali hiyo kuanzia kesho. Awali wafiwa walipewa Sh500,000

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza wafiwa wote waliopoteza ndugu kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere na watu 41 walionusurika kwenye ajali hiyo kupewa Sh1 milioni kila mmoja.

Awali, familia za waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo walipewa Sh500,000 kwa kila maiti.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu Septemba 24, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema kuanzia kesho wataanza kutoa kiasi hicho cha fedha zilizotolewa na Rais Magufuli kwa familia za marehemu na majeruhi wote.

“Rais ameniagiza niwaambie kwamba ameongeza fedha kwa waliopoteza ndugu zao, sasa watapata Sh1 milioni kila mmoja. Kuanzia kesho tutaanza kutoa fedha hizo pamoja na wale 41 walionusurika,” amesema Kamwelwe.

Waziri huyo amesema mpaka kufikia leo saa 12:10 jioni miili mingine miwili iliopolewa na kufanya idadi ya waliokufa kutokana na ajali hiyo kufikia 226.

Amesema kiasi cha fedha kilichokusanywa kutokana na ajali hiyo ni Sh397milioni zilizotolewa na watu mbalimbali.