Job Ndugai ndiye Spika wa Bunge la 11

Spika mpya wa Bunge la 11, Job Ndugai akivishwa joho la uspika mjini Dodoma leo

Muktasari:

Ndugai amepata kura hizo katika uchaguzi uliofanyika leo bungeni Dodoma ambapo alifatiwa na mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chadema, Goodluck Ole Medeye aliyepata kura 109 huku wagombea wengine sita wakipata kura 0.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kongwa (CCM) Job Ndugai ameshinda kiti cha Uspika kwa kura 264 sawa na asilimia 70 na hivyo kuwa Spika wa Bbunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndugai amepata kura hizo katika uchaguzi uliofanyika leo bungeni Dodoma ambapo alifatiwa na mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chadema, Goodluck Ole Medeye aliyepata kura 109 huku wagombea wengine sita wakipata kura 0.

Ndugai ambaye alikuwa Naibu Spika katika Bunge la 10 amesema kuwa anatambua dhamana aliyopewa hivyo kuwataka wabunge wote washirikiane kutimiza ahadi za Watanzania.

“Najua hali ya Watanzania, matarajio yao, umasikini wao. Najua nafasi ya chombo hiki katika kusimamia serikali ya Awamu ya Tano. Wabunge wote tushirikiane na kujenga upendo na ushirikiano,”amesema Ndugai.

Wengine waliogombea nafasi hiyo ni pamoja na Peter Sarungi wa AFP, Hassan Kisabia wa NRA, Dk Godfrey Malisa wa CCK, Richard Lyimo wa TLP, Robert Kisinini wa DP na Hashimu Rungwe wa Chaumma.