Joto la Nape, Bashe lampa tabu Bashiru

Muktasari:

Joto hilo likipanda, Dk Bashiru anasema hulazimika kutafuta maji na kulipooza.

Dodoma. “Wana joto la kupanda.”

Hivyo ndivyo anavyosema katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally anapowazungumzia wabunge wawili vijana wa chama hicho, Nape Nnauye na Hussein Bashe.

Joto hilo likipanda, Dk Bashiru anasema hulazimika kutafuta maji na kulipooza.

Akizungumza juzi jioni katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kizota mjini Dodoma, Dk Bashiru alisema wakati mwingine vijana wanakuwa na joto kali ambalo linahitaji kupozwa kwa kunywa maji.

“Wakati mwingine vijana mnakuwa na joto kali, hata kwenye Bunge kule nina vijana wenye joto kali mmoja anaitwa Bashe na mwingine anaitwa Nape. Kwa hiyo likipanda panda natafuta maji napozapoza,” alisema Dk Bashiru.

Hii ni mara ya tatu kwa katibu mkuu huyo wa chama tawala kutoa kauli hiyo akiwazungumzia Nape (mbunge wa Mtama) na Bashe wa Nzega Mjini.

Mara ya kwanza aliwazungumzia akiwa kwenye kampeni za Jimbo la Buyungu wilayani Kakonko mkoani Kigoma kisha mjini Nzega katika mkutano wa hadhara. “Kwa bahati nzuri mnaye mkurugenzi mchapakazi, mmeletewa mkuu wa wilaya mchapakazi, mbunge wenu, mwenyekiti wa CCM wilaya, katibu wa CCM Kata ya Kizota na mnaye Jamali Ngalya anayegombea katika kata hii. Wote hao ni vijana, sasa nyie vijana msituangushe maana wakati mwingine mnakuwa na joto,”alisema Dk Badhiru juzi.

“Sasa mwenyekiti wa CCM mkoa na wewe ushike maji ili joto la hawa vijana likipanda upozepoze, tena ushirikiane na mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Dk Binilith Mahenge) na mimi nitawasaidia maana ni mkazi wa Dodoma.”

Pamoja na hayo, Dk Bashiru alisema kuna mzee mmoja aliyedai kuwa, “anakejeli eti wanaohama Chadema kuhamia CCM wanadaiwa madeni, huo ni uongo.”

“Nyie mpuuzeni, yeye alipotoka CCM kwenda upinzani alikuwa na madeni kiasi gani na ni nani aliyemlipia?” alihoji.

Alisema wapo wanaowabeza wanaohama upinzani kwenda CCM na bahati mbaya wanaosema walikuwa CCM na kuhamia upinzani.

Dk Bashiru alisema Katiba ya nchi inamruhusu mtu kutumia haki yake ya kuchagua chama anachokipenda na si ya kununuliwa. “Wengine wanasema eti wanaokuja CCM wamenunuliwa, biashara ya kununua watu ilifanywa na wageni, kupitia biashara ya utumwa sasa kwa hayo maneno ni dharau, ni utovu wa nidhani siyo Uafrika wala Utanzania, mtu anatumia haki yake ya kikatiba kuchagua chama anachokipenda eti kanunuliwa, ana bei gani, nani mwenye bei hapa,” alisema.

“Sisi tunapambana na ufisadi na rushwa, tunapambana na umaskini, tunapambana kuongeza ajira na kulinda ajira za Watanzania, kulinda amani ya nchi hayo ndiyo yanayowaleta akina Jamali katika chama chetu.”

Alisema zamani CCM ililegea na watu walianza kukimbia, lakini sasa imejiimarisha ndiyo maana wanarudi.

Katika hatua nyingine, Dk Bashiru alisema vuguvugu linaloendelea kupitia uchaguzi mdogo wa marudio ni ishara ya kujaribu mitambo yao kwa ajili ya uchaguzi wa serikali ya mitaa mwakani na Uchaguzi wa Mkuu 2020.

“Hili linaloendelea mimi nawaambia sasa hivi tunajaribu mitambo, hivyo wakae chonjo mwaka kesho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, wakae chonjo 2020 na dalili inaonyesha mitambo inafanya kazi vizuri.”

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma Godwin Mkanwa alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa mkoa huo unaendelea kuwa ngome ya chama hicho.

Mgombea wa udiwani Kata ya Kizota (CCM), Jamali aliwaomba wananchi wamchague ili aendeleze yale aliyoyaanzisha akiwa diwani kwa tiketi ya Chadema.