Jubilee, Nasa wakataa makaratasi ya UNDP

Muktasari:

  • Jubilee wanasema nchi zinazoweza kusaidiwa ni zile zenye matatizo, vurugu
  • Nasa wanadai kwamba hizo ni mbinu za kutaka kurejesha kampuni wasiyoitaka
  • IEBC imesema haijafikia mwisho bali waendelea kujadiliana na kuingia mkataba

Uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais uliopangwa kufanyika Oktoba 26 unazidi kukumbwa na mawimbi makali hali inayotishia kuchelewa au kupangwa tarehe mpya kutokana na misimamo isiyotabirika ya chama tawala cha Jubilee na muungano wa Nasa.

Jana Jumanne maofisa wa Jubilee na Nasa walikataa mpango uliofikiwa kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) wa kugharimia uchapishaji wa makaratasi ya kura.

Msimamo huo ulifikiwa baada ya Ofisa mtendaji mkuu wa IEBC Ezra Chiloba kusema kuwa pendekezo la kutaka UNDP ibebe gharama za kuchapisha makaratasi ya kura ya urais bado lilikuwa likijadiliwa.

 

Kauli za vyama

Kiongozi wa walio wengi katika Bunge la Taifa Aden Duale alishutumu pendekezo hilo akidai kwamba ni kinyume cha sheria zinazohusu usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na akataka Wizara ya Fedha ipuuze pendekezo hilo.

“Kenya si nchi yenye matatizo. Mahali pekee ambako UN inaweza kwenda kuendesha chaguzi ni Haiti na Liberia,” alisema Duale bungeni. "Uchaguzi wowote utakaofanyika kutokana na fedha kutoka UN ni batili. Hii ni kwa kuwa huwa inataka kumridhisha mtu ambaye ni mroho wa madaraka.”

Duale alizungumza hayo alipoanzisha mjadala maalumu kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais uliojadiliwa kwa msingi kwamba ni suala la umuhimu mkubwa kitaifa.

Aidha, akizungumza na waandishi wa habari kutoka Capitol Hill yalipo makao makuu ya muungano wa Nasa, kiongozi wake mkuu na mgombea urais Raila Odinga alipinga pendekezo hilo na aliionya IEBC iache kujificha chini ya UNDP ili tu iipatie tena zabuni ya kuchapa makaratasi ya urais kampuni ya Al Ghurair Printing and Publishing yenye makao yake Dubai.

 “IEBC haiwezi kujificha chini ya UNDP ili isaidie katika uchapaji wa makaratasi ya kura. Hapa si suala la nani atalipa. Sisi tunapinga msaada huo,” alisema Odinga. Pia alisema madai kuwa IEBC iliingia mkataba wa miaka miwili na Al Ghurair hayana nguvu kwa kuwa wachapishaji hao walitafutwa na upande mmoja tu.

Alipotafutwa Chiloba kuhusu hilo alisema Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alitoa taaifa kuwa UNDP imejitokeza kusaidia upatikanaji wa karatasi. Msaada huo, alisema, unatokana na makubaliano ya kifedha yaliyofikiwa kati ya shirika hilo la UN na tume yake.

“Msaada huu unalenga kurejesha imani ya watu na kuaminika kwa makaratasi pamoja na fomu za kujumlishia matokeo yatakayotumika kwenye uchaguzi wa marudio pamoja na kuzingatia utatuzi wa matatizo yaliyoibuliwa katika hukumu ya Mahakama ya Juu,” alisema Chebukati.