Kashfa ya hosteli mpya UDSM, polisi yamshikilia mwanafunzi

Muktasari:

Mabweni hayo yanayotumiwa na wavulana katika jengo la Block A yana nyufa sehemu mbalimbali kuanzia chini hadi ghorofa ya tatu.

       Dar es Salaam. Nyufa zilizoonekana katika mabweni mapya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zimezua mjadala na kuingiza wanafunzi hofu kwa kuwa majengo ni mapya na yamejengwa kwa gharama kubwa.

Mabweni hayo yanayotumiwa na wavulana katika jengo la Block A yana nyufa sehemu mbalimbali kuanzia chini hadi ghorofa ya tatu.

Akizungumza na Mwananchi mbunge wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo (Daruso), Simon Masenga alisema nyufa hizo zilianza kuonekana wiki mbili zilizopita.

Alisema walitoa taarifa kwa meneja wa hosteli lakini majibu waliyopewa ni kuwa majengo hayo yako chini ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Mbunge mwingine wa serikali ya wanafunzi, Kumbusho Dawson alisema majengo hayo yana upungufu, ukiwemo wa maji kutuama kwenye bafu na kutokuwa na makabati.

“Tumelalamika kwa meneja wa mabweni kuhusu upungufu katika majengo haya na majibu tunayopewa ni kuwa bado yako chini ya TBA,” alisema Dawson.

Majengo hayo yaliyojengwa na TBA kwa miezi minane yakielezwa kugharimu Sh10 bilioni yalizinduliwa Aprili 15, 2017.

Ujenzi ulifanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kumaliza tatizo la malazi kwa wanafunzi wa UDSM.

Akizungumzia nyufa hizo jana Mtendaji Mkuu TBA, Mhandisi Elius Mwakalinga alisema walizitarajia kwenye jengo moja la Block A na hazina madhara.

Alisema nyufa katika jengo hilo la hosteli ambalo ni kati ya sita yaliyopo Block A zimetokea eneo walilotarajia ambalo kitaalamu linajulikana (expansion joint) hivyo hazina madhara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwakalinga alisema kwa kawaida udongo unaobeba jengo hutitia baada ya muda fulani, hivyo wakati wa ujenzi huacha nafasi kuliwezesha jengo kupumua bila kusababisha nyufa.

Mwakalinga amesema kuna makosa yalifanyika ya kuziba nafasi zilizoachwa (expansion joint) kwa kutumia saruji badala ya mbao au plastiki maalumu hivyo kuonyesha nyufa kwenye jengo hilo.

Alisema nyufa zimetokea sehemu mwafaka ambazo walitarajia na kwamba kila jengo lina expansion joint tatu kwa ajili ya usalama wa jengo.

Mwakalinga alisema majengo hayo ya hosteli za wanafunzi bado yako chini ya uangalizi wa TBA, kwa hiyo wataanza ukarabati na hakuna haja ya kuhamisha wanafunzi kwa sababu jengo liko imara.

Alisema kwa taaluma ya ujenzi wa majengo, dosari hiyo ni ya kawaida kutokea na kwamba, wakala umeanza kuchukua hatua kuzisahihisha kwa kuhakikisha uwazi uliopo unakuwa huru bila kujazwa kitu kigumu.

Mwakalinga alisema ujenzi umegharimu Sh10 bilioni walizopewa na Serikali na kwamba fedha hizo zilitosha kwa sababu walizingatia hadidu za rejea walizopewa na Rais Magufuli kwa ajili ya ujenzi.

Alisema wamejenga vyumba 960 vyenye uwezo wa kubeba wanafunzi 3,840 na kwamba, gharama ya vyumba hivyo ni sawa na Sh10.4 milioni kwa kila kimoja.

Mwakalinga alisema Sh10.8 bilioni zimetumika kujenga shule ya Ihungo mkoani Kagera iliyobomoka kutokana na tetemeko la ardhi ambayo itakuwa na nyumba 30 za walimu.

“Walijitokeza watu kujenga kwa Sh60 bilioni lakini sisi tumejenga kwa Sh10 bilioni tu. Kwa hiyo, inawezekana na sisi ndiyo tuliojenga, msiwasikilize wengine ambao hawana ujuzi wowote katika ujenzi,” alisema.

Akizungumzia muda wa ujenzi, alisema hosteli hizo zilijengwa kwa miezi minane ambayo kitaalamu inatosha kwa ujenzi imara.

Alisema msingi wa mabweni hayo una uwezo wa kubeba ghorofa nyingine mbili zaidi na utaalamu ulizingatiwa katika ujenzi.

Maelezo hayo ya Mwakalinga yamepingwa vikali na wananchi waliokuwa wakitoa maoni yao kwenye kurasa zao za facebook. David Mtowe alijohi, “Kama walitarajia kuna tatizo mahali, wawajibishwe, mbona majengo makubwa zaidi ya hayo hayana hizo nyufa! na yakimaliza miaka kumi hali itakuwaje?”

Anaandika Gidion G Mula kuwa , “Siku ya uzinduzi mbona hamkusema kama nyufa zitajitokeza zenye ukubwa wa kiwango cha mlango tukajua eeeeh.”

Saulo Sawila ameandika “Tukiingiza lugha rahisi katika mambo mazito tujiandae kuishi kwa kuanza kuamini hatuwezi kukosea mpaka tuharibu kabisa

Kwa mtazamo wangu finyu hii ndio mamlaka yenye kusimamia majengo ya Serikali kuhakikisha wanayapokea katika ubora unakubalika inapotokea mhandisi mkaguzi mwenye dhamana ya mwisho kutumia lugha rahisi kwa maswali magumu akiamini uelewa watu wa ni finyu kwa kiwango cha kushindwa kutofautisha nyufa na za kutitia kwa jengo na ubora wa jengo ni hatari sana.”

Faraji Majora aliandika, “Wangesema tu jengo limejengwa chini ya kiwango ni maneno machache ila yana maana wananchi tungewaelewa!”

Mhandisi mmoja wa ujenzi ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema kutokana na jinsi nyufa zile zilivyonyooka tatizo la majengo hayo ni kuwa vifaa vya ujenzi, hasa matofali, havikuwa vyenye ubora.

Alisema iwapo matofali yangekuwa na ubora unaotakiwa nyufa zingekuwa zinapinda kuyafuata, tofauti na hali ya sasa ambayo inawezekana tu kama limepita tetemeko la ardhi.

Mhandisi huyo alisema vilevile nyufa hizo zinaonyesha kwamba jengo hilo limetitia upande kutokana na upungufu katika msingi wake, na hivyo kutokuwa salama sana kwa matumizi.

“Inaonekana hata usimamizi wa ujenzi haukuwa mzuri, ndio maana hata vifaa vya ujenzi vikakosa ubora unaotakiwa,” alisema mhandisi huyo.

UDSM yaunda kamati kuchunguza

Wakati mjadala ukiendelea UDSM imeunda kamati maalumu ya kuchunguza majengo ya hosteli hizo.

Meneja wa hosteli hizo, Josephat Buhenyenge amesema kamati hiyo inaundwa na wahandisi mbalimbali ambao wataangalia kama nyufa zinazoelezwa zinaweza kusababisha madhara.