Katambi, mwenyekiti Bavicha aliyetoka kama alivyoingia

Muktasari:

Katambi, aliyechanguliwa kuwa mwenyekiti Bavicha Septemba 11, 2014 akichukua nafasi iliyoachwa na John Heche, hakuwa anategemewa kama angeweza kuaminiwa na vijana kushika wadhifa huo.

Dar es Salaam. Aliingia bila kutegemewa na ameondoka bila kudhaniwa.

Ndivyo unavyoweza kuelezea uamuzi wa aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi kujiunga na CCM jana.

Katambi, aliyechanguliwa kuwa mwenyekiti Bavicha Septemba 11, 2014 akichukua nafasi iliyoachwa na John Heche, hakuwa anategemewa kama angeweza kuaminiwa na vijana kushika wadhifa huo.

Na hakutegemewa kama angeiacha jumuiya hiyo siku chache baada ya kusimama jukwaani kusisitiza msimamo wake mbele ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Na hakutegemewa kuwa angepewa nafasi adimu ya kuzungumza mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), tena katika kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, kutangaza tu uamuzi wa kujiunga na chama hicho.

Lakini yote yamewezekana.

Katika uchaguzi wa Bavicha 2014, Katambi alipambana na Daniel Naftali na Upendo Peneza waliokuwa wakipewa nafasi kubwa, lakini sarakasi za hapa na pale ziliwatupa nje.

Nguvu ya Katambi haikuwa kubwa kutokana na ugeni wake ndani ya Chadema, ikilinganishwa na Naftali pamoja na Peneza.

Lakini aliibuka kidedea akikusanya kura 173 wakati aliyekuwa mshindani wake mkubwa, Peneza akipata kura 70 katika uchaguzi wa ng’we ya pili baada ya awali uliohusisha wagombea 13 kushindwa kupata asilimia 50 ya kura zote 243.

Mara baada ya kutangazwa mshindi na msimamizi wa uchaguzi huo, Roderick Lutembeka ambaye ni katibu mkuu wa Baraza la Wazee Chadema, Katambi aliwashukuru wote.

“Makundi yameisha hapa leo. Nawashukuru walionipa kura lakini hata walioninyima, twendeni tukaijenge Bavicha yetu iwe imara,” alisema.

Kabla ya ngwe ya pili, maneno dhidi ya Katambi yalipamba moto mitandaoni na kusababisha kuwe na makundi mawili makubwa yaliyowalazimu viongozi wawili wa juu, Mbowe na katibu mkuu wa wakati huo, Dk Wilbroad Slaa kufika ukumbini usiku wa manane kutuliza hali.

Katambi, aliyekuwa mwanasheria wa kampuni za Sahara Media Group inayomilikiwa na mwenyekiti wa CCM wa Mwanza, Anthony Diallo alionekana kama amepandikizwa na chama hicho tawala, huku Peneza akihusishwa na mfanyabiashara mmoja maarufu nchini.

Saa 8.47 usiku baada ya wagombea 13 kumaliza kujinadi, Mbowe alilazimika kutoa neno la kuweka mambo sawa ili kuhakikisha vijana hao wanamchagua kiongozi wao pasipo vishawishi.

Mbowe aliwataka vijana hao kuacha siasa za kuchafuana katika mitandao ya kijamii.

“Nimefanya juhudi sana kukijenga chama hiki. Ninaumia kuona watu wanaotaka uongozi, wanachafuana kupitia mitandao ya kijamii,” alisema Mbowe.

“Kila mtu anataka kuwa kiongozi lakini si kwa kuchafuana. Mnachafuana katika mitandao, mnakidhalilisha chama na mnakivua nguo chama chenu. Huo ni uhuni.

“Mtakapomaliza uchaguzi tokeni na umoja, wekeni makundi kando, nendeni mkaijenge Bavicha na Chadema yenu. Sitaki makundi. Yaliyoifikisha CCM hapo ni makundi sasa hatutaki kuona yanajitokeza kwetu.”

Hata hivyo akizungumza na Mwananchi kuhusu kuhama kwa Katambi na kile kilichojitokeza katika uchaguzi wa Bavicha jana, Peneza alisema amefanya uamuzi katika kipindi kinachohitaji wenye roho ngumu.

“Katambi ni kijana mwenzetu ambaye tumeshirikiana na tulishindana katika uchaguzi, lakini alichokifanya ni uamuzi wake,” alisema.

“Ameufanya katika kipindi ambacho (wanahitajika) wenye roho ngumu bila kuogopa vitisho na kukamatwa. Katika harakati hizi unahitaji wenye moyo.”

Pendeza alisema wakati wa uchaguzi wa Bavicha, Suala la jinsia lilimnyima uenyekiti.

“Lakini chama kilitambua umuhimu wangu mwingine na kunipa nafasi hii ya kuwatumikia Watanzania,” alisema.

“Hata kama kuna watu wanasema Katambi alibebwa, basi angeonyesha utofauti lakini alishindwa. Bavicha aliirudisha nyuma.”

Katambi alivyobadilika ghafla

Katika mkutano wa kampeni za udiwani uliofanyika Novemba 14 mjini Masasi, Katambi alipanda juwaani akiwa pamoja na Mbowe na alichokisema ni tofauti na alichofanya siku saba baadaye mbele ya mwenyekiti wa CCM, John Magufuli.

“Mambo mengi yalikuwa mrama na watu tunapenda mabadiliko ila hatutaki kubadilika. Kama nitaitwa msaliti basi nitakuwa msaliti kundi la wasaliti wa nchi hii, ukombozi ulishapatikana, siyo tunachokisema majukwaani ndiyo tunachokiamini,” alisema baada ya kupewa nafasi na mqwenyekiti huyo wa CCM jana.

Lakini Novemba 14, Katambi alisema huu ni wakati ambao vyama vinapita kujinadi kila kimoja na ahadi zake.

“Ahadi zetu tulizoziahidi zote tunazitekeleza hasa za kusimamia Serikali na kwamba mngetupa Serikali tungehakikisha tunaboresha maisha ya Watanzania bila uongo,” alisema.

“Lakini baadhi yenu pengine walichagua CCM, sasa ni wakati kwa wale waliochagua CCM kujisahihisha. Mtu unapojisahihisha maana yake unaonyesha hasira kwenye mambo makubwa matano ambayo nataka niyazungumze.

“Jambo la kwanza, kunja kidole cha kwanza tusema tulidanganywa, tuliambiwa Sh50 milioni zinakuja, hazijaja. Tuna hasira, tunaanza kukunja ngumi taratibu.

Pia alizungumzia upatikanaji dawa kwa kila mtu, hasa watoto na wazee.

“Hao wamedanganywa. Kunja kidole cha pili tunaelekea kwenye ngumi kumpandisha CCM kuonyesha hasira,” alisema.

“Tatu, tunasema kwamba sasa nchi hii hali ni mbaya. Njaa balaa, mtu anadaiwa benki, kwenye kilimo, amekopa Voda, amekopa Tigo, kila sehemu ana madeni. Njaa ni kali. Kunja ngumi.

“Nne, kuonyesha kwamba haya waliyotuahidi wameonyesha sifa kuu za mnafiki kwanza akiahidi hatekelezi, pili akisema jambo anasema uongo na mwisho ukimwamini haaminiki anafanya hiana.

Pia aliwataka wakumbuke kutoipigia kura CCM.

“Tunakunja kidole cha tano kwa sababu tunataka kuonyesha CCM kwamba Serikali hii sio ya CCM wala sio ya mtu mwingine yeyote,” alisema.