Kenyatta aapishwa, aahidi kuteta na viongozi wa kisiasa

Muktasari:

Rais Kenyatta ametangaza mtu yeyote kutoka nchi ya Afrika anayekwenda Kenya kwa shughuli yoyote sasa atapewa viza akifika mpakani au akiwasili kwenye viwanja vya ndege nchini Kenya.

Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta ameapishwa kuongoza Kenya kwa muhula wa pili wa miaka mitano na wa mwisho katika sherehe zilizofana na ameahidi katika hotuba yake kuondoa viza na kukutana na wanasiasa kwa masilahi ya Kenya.

"Naapa kwamba nitakuwa mwaminifu na mtiifu kwa Jamhuri ya Kenya; kwamba nitatii, nitahifadhi, nitalinda na kutetea Katiba ya Kenya kwa kuzingatia sheria, na nitazingatia sheria zote; na kwamba nitalinda na kusimamia kikamilifu utaifa, uadilifu na heshima ya watu wa Kenya,” alisema Kenyatta huku akiwa ameshika Biblia kwa mkono wa kulia alipokuwa akila kiapo cha kuingia ikulu.

Biblia hiyo, kwa mujibu wa Mkuu wa sherehe Duncan Okello, ni ileile iliyotumiwa na rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta aliyoishika wakati wa uhuru Desemba 12, mwaka 1963.

Hatua ya Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto kula kiapo ina maana Kenya imekamilisha shughuli za kupata viongozi ikiwa ni baada ya siku 123 tangu ulipofutwa uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.

Katika uchaguzi huo Kenyatta alipata ushindi wa asilimia 54 na kumwangusha mshindani wake Raila Odinga wa muungano wa Nasa aliyeshika nafasi ya pili akiwa na asilimia 44. Hata hivyo Odinga alifungua kesi Mahakama ya Juu kupinga ushindi huo na baada ya kupeleka ushahidi uchaguzi huo kwa kura ya urais ulifutwa.

Uchaguzi wa marudio uliopangwa Oktoba 26 ulisusiwa na Odinga aliyedai hayakufanyika marekebisho katika mfumo ili uwe wa haki na wa kuaminika. Kujiondoa kwake kulimwacha Kenyatta akijinyakulia ushindi wa asilimia 98 huku asilimia 38 tu ya wapigakura 19.6 milioni waliojiandikisha wakishiriki.

Maelfu ya watu walihudhuria sherehe hizo wakiwemo wakuu wa nchi na watu mashuhuri wapatao 40. Wahudhuriaji, wengi wao wakiwa wafuasi wa chama tawala cha Jubilee, walishangilia kwa nguvu, waliimba na kucheza katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kasarani.

 

 

Kukutana na wanasiasa

Kwa kuwa uchaguzi huo umesababisha mgawanyiko mkubwa, mara baada ya kula kiapo cha utiifu, Kenyatta aliahidi mambo kadhaa likiwemo la kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa na kuwaelezea nia yake ya kuendeleza umoja.

Kenyatta alisema ana malengo ya kuimarisha uwiano na umoja miongoni mwa Wakenya na akadokeza kwamba siasa zimetumiwa vibaya kutatiza ustawi wa taifa "badala ya ilivyo nchi za Asia." “Hakuna aliyewahi kula siasa," alisema.

Vile vile aliahidi “kutenda haki kwa watu wote kwa kuzingatia Katiba, kwa sheria, kuheshimu sheria bila woga, upendeleo, uswahiba wala inda.”

Kenyatta amewahimiza Wakenya kuishi kama majirani kwani hufaana sana na hutegemeana wakati wa shida.

 

Viza

Rais Kenyatta ametangaza mtu yeyote kutoka nchi ya Afrika anayekwenda Kenya kwa shughuli yoyote sasa atapewa viza akifika mpakani au akiwasili kwenye viwanja vya ndege nchini Kenya.

Rais alisema hataweka masharti kwamba lazima mataifa mengine yafanye hivyo lakini ameiga mfano wa Rwanda (yenyewe ni raia yeyote wa nchi yoyote) ambayo ilichukua hatua hiyo hivi karibuni.

Kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kenyatta amesema atashirikiana na viongozi wa EAC kufufua moyo wa Jumuiya hiyo kwamba wananchi wa nchi wanachama watahesabiwa kama Wakenya; watahitajika tu kutumia kitambulisho.

Amesema wananchi kutoka nchi za EAC wanaweza kuingia au kutoka na kufanya kazi, kumiliki mali au hata kuoana bila kuwekewa masharti.

 

Sheria

Kuhusu mahakama alisema watazungumza na idara hiyo kuhusu kuharakishwa kwa kesi ambazo zimekwama miaka mingi na nyingi nyingine ambazo zinatumiwa kukwamisha miradi ya serikali.

"Sheria lazima itawale. Inafaa kuwa kimbilio kwa kila Mkenya na hakuna mtu yeyote kuvunja sheria au kwenda nje ya mfumo wa sheria bila kujali ukubwa wa malalamiko yako,” amesema.

"Naomba niwakumbushe kwamba, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilipotutaka tujitee, tulitii. Mahakama ya Juu ya Kenya ilipofuta uchaguzi wetu, hata baada ya kushinda, baada ya kuambiwa utaratibu ulikuwa muhimu kuliko kura, tuliheshimu uamuzi huo. Serikali yangu imedhihirisha kujitolea kuheshimu sheria. Tunatarajia raia wote wengine wafanye hivyo," amesema.

Kuhusu Katiba amesema ndiyo iliyounda mihimili mitatu huru ya serikali na akata kila mmoja ufanye kazi yake. "Matamanio ya binadamu wakati mwingine huzidi kipimo, na yasipodhibitiwa yanaweza kulibomoa taifa. Ili kuishi pamoja, lazima watu wakubaliane kufuata sheria fulani. Kenya ni nchi ya watu zaidi ya 40 milioni. Tumeishi pamoja ishara kwamba hata tukitofautiana huwa tunajua namna ya kuungana tena.”

Alisema kwa pamoja, bila kujali tofauti za kidini na za kijamii, Wakenya wanaweza kujenga Kenya imara na lenye ustawi.

Ruto

Vilevile, Makamu wa Rais William Ruto aliapishwa katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na wakuu wa nchi za Afrika Mashariki; Hailemariam Desalegn (Ethiopia), Paul Kagame (Rwanda), Mohamed Abdullahi Mohamed (Somalia), Salva Kiir (Sudan Kusini), Ian Khama (Botswana) na Yoweri Museveni (Uganda).