Abiria ashushwa baada ya kuiombea ndege ipate ajali

Muktasari:

  • Rubani alilazimika kutoa taarifa kwa polisi waliokuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Islamabad nchini Pakistan

Islamabad, Pakistan. Mtu mmoja ameshushwa kwenye ndege iliyokuwa ikisafiri kwenda Dubai, wakati alipoanza kufanya maombi na kumtaka Mungu wake kusababisha ajali ya ndege hiyo, kabla ya kuanza  safari kutoka Pakistan.

Abiria huyo ambaye alitambuliwa kwa jina moja la Khalil inadaiwa alianza maombi yake hayo punde tu alipoketi ndani ya ndege hiyo ikiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Islamabad.

Maombi yake yaliwafanya abiria kuanza kuingiwa na hofuhasa wasafiri na wahudumu wa ndege waliokuwapo.

Khalil alikuwa akisafiri kuelekea Australia kupitia Dubai na alikuwa ndiyo kwanza amepanda ndege hiyo jijini Islamabad.

Baada ya kusikia maombi hayo, rubani wa ndege hiyo alitoa taarifa idara ya ulinzi katika uwanja huo kufuatia maombi ya kushangaza ya msafiri huyo.

Baada ya kutoa taarifa polisi waliokuwapo kwenye uwanja huo walilazimika kumshusha ndani ya ndege hiyo.

Hata hivyo, jina lake kamili halikutambuliwa, wala kampuni ya ndege ambayo alikuwa akitumia kusafiri.

Novemba 2018, abiria mwingine aliyekuwa amekasirika alichoma mizigo yake baada ya safari yake kufutwa akiwa kwenye uwanja huohuo wa ndege.

Abiria huyo inadaiwa alikasirishwa na taarifa za  kuzuiwa kuruka kwa ndege aliyokuwa aondoke nayo ya kampuni ya Pakistan International Airlines (Pia) kutokana na hali mbaya ya anga iliyokuwapo.

Msafiri huyo alirekodiwa video akiteketeza mizigo yake, nguo na vitu vingine katika uwanja huo wa Islamabad kabla ya polisi kumzuia.