Bobi Wine: Tuna nguvu kumkabili Rais Museveni

Mbunge wa Kyadondo Mashariki nchini Uganda, Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine amesema ana matumaini ya upinzani kumpa ushindani mkali Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa 2021.

“Kuwa na vijana 85 ya watu nchini Uganda ni matumaini mapya. Na sio vijana tu, hata watu wazima pia wanatuunga mkono na kwamba watu wa Uganda sasa wameungana zaidi ya ilivyokuwa awali. Hivyo basi ndiyo nimesema awali na nasema tena sasa kwamba kundi langu nami tutakabiliana na Rais Museveni katika uchaguzi utakaofanyika baada ya miaka mwili kutoka sasa,” alisema,

Akizungumza katika mahojiano yaliyochapishwa na Mtandao wa The Citizen, Bobi Wine alisema ingawa hawajafikia uamuzi wa mwisho, wanajaribu kuwaleta watu pamoja na nguvu zote zinazopigania mabadiliko kwa lengo la kuingia katika uchaguzi huo wakiwa kitu kimoja.

“Ndio tumezungumza lakini tuko wengi wanaotaka kuwania. Mmoja wetu kati yetu atachaguliwa na kupewa baraka kutuongoza na nasema iwapo kundi hilo litanipatia bendera mimi kuongoza, niko tayari kushindana na Museveni,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kiwango cha wafuasi wake tangu aingie siasa alisema kuwa hakushangaa kutokana na miaka mingi aliyohudumu kama mwanamuziki.

 

Sera za miaka 33

Bobi Wine alisema atatekeleza ajenda 10 za Rais Yoweri Museveni ambazo amekuwa akijaribu kuzitekeleza katika kipindi chake chote cha miaka 33.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa sera yake itakuwa utekelezaji wa ajenda hizo kwa kuwa hakuna hata moja ambayo imetekelezwa hadi sasa.

Bobi Wine amesema utekelezwaji wa sera hizo umekumbwa na matatizo kutokana na ufisadi na sheria mbovu.

Kwa mujibu wa Bobi Wine, taifa hilo limekuwa na maono mengi kama vile Vision 2040 na mengine mengi ambayo yamewasilishwa na kuwekwa kando.

“Ndio tumekuwa na mipango mingi ikiwemo ule wa Vison 2040 na mengine mengi. Haijatekelezwa kutokana na ufisadi mwingi. Hivyo basi lengo letu ni kutekeleza sera na mipango ambayo imependekezwa katika siku za nyuma,” alisema.

Alisema: Lazima ifahamike kwamba Uganda haijakosa sera nzuri. Tumekuwa na mapendekezo chungu nzima na mengi yamefanyiwa utafiti wa hali ya juu na kuwasilishwa.

 

Waganda wanataka mabadiliko 

Bobi Wine anasema katika mikutano yake raia wengi wamekuwa wakishinikiza mabadiliko ijapokuwa wanasiasa wengi ambao wamekuwa wakijitokeza wamekuwa wakinunuliwa na wengine wakitishiwa.

Alipoulizwa kuzungumzia kuhusu hali iliyopo Sudan, Bobi Wine alisema kuwa hali hiyo inaonyesha wazi kwamba raia wamechoshwa na uongozi wa kiimla.

''Ni sharti ikumbukwe kwamba al-Bashir alikuwa dikteta mkubwa, alikuwa na jeshi kubwa zaidi ya Museveni lakini aliondolewa na uwezo wa raia. Hivyo basi hilo linatupatia moyo wa kuamini na kuendelea kupigania demokrasia katika taifa letu.”