EU, AU wampa baraka zote Tshisekedi

Wednesday January 23 2019

 

Brussels, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wametangaza kutambua uamuzi wa Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumtangaza, Felix Tshisekedi kama Rais halali wa nchi hiyo baada ya kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) kufuatia uchaguzi mkuu wa Desemba 30 mwaka jana.

Taasisi hizo zimesema zipo tayari kushirikiana na kiongozi huyo mteule anayetarajiwa kuapishwa kesho katika mji mkuu wan chi hiyo Kinshasa, sherehe ambazo zinatarajiwa kufanyika kwenye uwanja wa mpira.

Viongozi wa EU na AU wamesema wamejadiliana kuhusu matokeo ya uchaguzi huo katika mkutano wao mjini Brussels na keleza uungaji mkono uamuzi wa Mahakama kwa Tshisekedi.

Hata hivyo, maofisa hao katika mkutano na waandishi habari hawakusema wazi hadharani kwamba wanamtambua Tshisekedi kama mshindi na hata hawakumpongeza.

Mkuu wa Sera za Mambo ya Nje wa UN, Federica Mogherini aliwaambia waandishi habari pamoja na wajumbe wa AU kuwa changamoto zinazomsubiri Rais mpya wa Congo ni nyingi katika masuala mbalimbali na yote hayo yanamhitaji awe nguvu ya kuunganisha.

"Rais huyo anatarajiwa kukabili changamoto nyingi nchini mwake zikiwamo masuala ya uchumi, ulinzi, kijamii na utawala bora.’’

"Haya yote kiongozi huyo anatarajiwa kukabiliana nayo kwa pamoja ikiwa ni kutoka nje ya nchi kuonana na watu mbalimbali wakiwamo wanasiasa  na wataalamu wa uchumi ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi,’’ alisema Mogherini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Richard Sezibera alisema AU imetambua matokeo kamili ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Mahakama ya Katiba.  “Umoja wa Afrika bado una nia ya kuendelea na ushirikiano na raia wa DRC ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza," alisema  Sezibera.

Advertisement