Google yaibania Huawei kutumia Android

Muktasari:

  • Hatua ya Google kuibania Huawei inadaiwa kuchangiwa na mgogoro wa kibiashara ulioibuka baina ya Marekani na China

 

Mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na China umeingia hatua nyingine baada ya kampuni ya Google ya Marekani kuizuia Huawei ya China kutumia baadhi ya huduma kwenye mfumo wa uendeshaji wa Android.

Kutokana na uamuzi huo, simu mpya za Huawei hazitakuwa na baadhi ya app zinazohusiana na Google.

Hii ni baada ya uongozi wa Trump kuiongeza Huawei katika orodha ya kampuni ambazo Marekani haitafanya nazo biashara hadi ziwe na leseni maalumu.

Katika taarifa yake Google imesema “inatekeleza maagizo na inapitia madhara yake” Huawei imekataa kuzungumzia suala hilo.

Hii ina maana gani kwa watumiaji?

Watumiaji wa sasa wa simu za Huawei wanaweza kuhuisha app na mifumo yake ya kiusalama na pia kuhuisha mfumo wa huduma ya Google Play, lakini baada ya zuio, mambo yatakuwa tofauti.

Google itakapozindua Android mpya baadaye mwaka huu, inawezekana isiwepo katika simu za Huawei.

Kwa mujibu wa BBC, vifaa vya Huawei vya baadaye vinaweza visiwe na huduma kama za YouTube na Ramani.

Ben Wood, wa CCS Insight Consultancy, amesema hatua hiyo itakuwa na  athari kubwa kwa biashara ya Huawei.

Mara baada ya Marekani kuiweka Huawei katika orodha ya kampuni zinazotakiwa kuwa na leseni maalumu kufanya biashara ya Marekani, mtendaji wake mkuu, Ren Zhengfei aliviambia vyombo vya habari vya Japan kuwa “walikuwa wamejiandaa kwa hatua hiyo”.

Alisema kampuni hiyo ambayo hununua vifaa vya karibu Dola 67 bilioni kila mwaka, itaanza kusonga mbele kwa kutengeneza vya kwake.

Huawei inapata upinzani mkubwa kutoka nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kuhusu mtandao wake mpya wa 5G.

Nchi kadhaa zimelalamika kuwa mtandao huo unaweza kutumiwa na China kwa ujasusi, madai ambayo Huawei imeyakanusha.

Pamoja na kuwa imesema mtandao wake hauna tishio lolote  na yenyewe iko huru kwa Serikali ya China, baadhi ya nchi, ikiwamo Uingereza zimezuia bidhaa za Huawei zinazotumia 5G.