Julian Assange bado yuko mikononi mwa dola

Muktasari:

  • Muasisi wa mtandao wa WikiLeaks, Julian Assange aliyekamatwa katika ubalozi wa  Equador mjini London Uingereza bado yuko mikononi mwa vyombo vya dola huku waandamanaji wakianza kujitokeza barabarani kutaka aachiwe huru

London, Uingereza. Muasisi wa mtandao wa WikiLeaks, Julian Assange aliyekamatwa katika ubalozi wa  Equador mjini London Uingereza bado yuko mikononi mwa vyombo vya dola huku waandamanaji wakianza kujitokeza barabarani kutaka aachiwe huru.

Assange,  raia wa Australia  anakabiliwa na na mashitaka nchini Marekani ya kufichua siri za serikali. Wakionyesha kutokubaliana na kukamatwa kwake, harakati za kumuunga mkono Assange zimeanza katika nchi alikozaliwa Australia.

Watu wasiopungua 30 waliandamana katika eneo la kati ya Sydney baada ya kukusanyika nje ya ubalozi mdogo wa Uingereza na kutoa wito aachiliwe huru yule wanaemtaja kuwa "mshika bendera wa wanaopigania ukweli na uhuru wa mtu kuzungumza”.

Wakibeba maaandishi yanayosema "Aachiwe huru Assange. Asipelekwe Marekani,"waandamanaji hao wamedai pia Assange "msema kweli aachiwe huru na mjumbe asipigwe risasi". Kundi jingine dogo la watu wameandamana katika mji wa Melbourne.

Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison amesema  nchi yake haihusiki na mipango ya kumpeleka Marekani na kwamba Assange atapatiwa huduma za kawaida na maofisa wa ubalozi mdogo wa Australia.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Marise Payne akijibu hofu za mashabiki wa Assange kuhusu uwezekano wa adhabu atakayopewa nchini Marekani, amesema Australia inapinga moja kwa moja adhabu ya kifo.

Ameongeza kusema Uingereza imetaka ihakikishiwe na Marekani kwamba Assange hatohukumiwa adhabu ya kifo pindi akipelekwa nchini humo.