Kampuni yaruhusiwa kusambaza vyakula, vinywaji kwa kutumia ndege ndogo za drone

Wednesday April 10 2019

 

Canberra, AFP
Kampuni yenye uhusiano na Google itaanza kutoa huduma za vyakula na bidhaa nyingine ndogo kwa wakazi wa Canberra kwa kutumia ndege ndogo zisizo na rubani (drone) baada ya kupata ruhusu ya mamlaka inayosimamia usafiri wa anga.
Kampuni inayojulikana kwa jina la Wing Aviation Pty Ltd, ambayo ni kampuni ndogo ya Alphabet inayomilikiwa na Google, imekuwa ikifanya majaribio ya kusambaza bidhaa kwa miezi 18 iliyopita, lakini sasa itaweza kuendelea kikamilifu na shughuli hizo.
"Tumeiruhusu Wing Aviation Pty Ltd kufanya shughuli inazoendelea nazo za ugavi wa bidhaa CanBerra Kaskazini," Mamlaka ya Usalama wa Anga ilisema jana.
Kampuni hiyo ilisema imekuwa ikisambaza "vyakula na vinywaji vya viwandani, kahawa inayopikwa kienyeji na chokoleti".
Kampuni hiyo ilisambaza huduma mara 3,000 na hivyo kuwshawishi mamlaka kuwa mradi huo ni salama na hivyo kuipa kibali cha kufanya biashara hiyo nchini Australia, ikiwa ni ya kwanza duniani.
Ndege hizo zenye mabawa zitaruhusiwa kuruka kwa saa 11 hadi 12 na ni lazima ziongozwe kwa rimoti, kuliko kuachwa kufanya kazi bila ya msaada.
Eneo la awali la kufanyia biashara litahusu nyumba 100, lakini idadi hiyo inatarajiwa kukua.
Mamlaka ya usimamizi haikuzingatia suala la kelele za ndege hizo au faragha, mambo mawili yaliyoibuka wakati wa majaribio.
Wing inasema kuwa usambazaji bidhaa kwa njia ya ndege hizo unapunguza foleni za magari, uchafuzi wa hewa na pia huduma hutolewa kwa haraka -- ndani ya dakika kumi baada ya maombi.
Mteja hutumia app kuagiza bidhaa, ambayo hupakiwa kwenye ndege hiyo kwa ajili ya kupelekewa.
Ndege hiyo huenda hadi sehemu bidhaa ilikoagizwa na kushusha mzigo yenyewe kabla ya kupaa kuondoka. AFP

Advertisement