Malawi wapitisha sheria kuzuia takrima uchaguzi mkuu

Muktasari:

  • Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika Mei mwakani unatarajiwa kuwa mgumu katika historia ya Malawi kutokana na Rais wa zamani wa nchi hiyo mwana mama, Joyce Banda kuchuana na Rais wa sasa, Peter Mutharika.

Lilongwe, Malawi. Malawi imepitisha sheria inayopiga marufuku wanasiasa kutoa fedha na takrima nyingine kama kivutio ili kupata kura katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika Mei mwakani.
Mwanasiasa yeyote ambaye atakiuka sheria ya vyama vya siasa ambayo ilianza kutumika Jumamosi iliyopita, atakabiliwa na faini ya kwacha 10 milioni (dola za Marekani 13,000) au kifungo cha miaka mitano jela.
Hata hivyo, vitu kama mabango ya kampeni, vipeperushi na nguo havijaguswa katika sheria hiyo mpya.
Malawi itafanya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani Mei 21 mwakani na wagombea katika kila ngazi wamekuwa wakiwapa fedha na zawadi wapigakura ili kushawishi kuungwa mkono.
Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Malawi, Henry Chingaipe ameiambia AFP kwamba sheria hiyo mpya itasaidia kuweka usafi katika siasa za Malawi.
“Tumeeneza utamaduni wa siasa za urithi kupitia takrima, badala ya watu kupiga kura kwa kufuata dhamiri, ukweli unanunua kura," alisema.
Rais wa zamani, Joyce Banda kutoka chama cha Peoples Party (PP) amesema: "Tunapaswa kuzingatia kile kinachosemwa,".
Uchaguzi wa Mei unatarajiwa kuwa muhimu zaidi katika historia ya Malawi kwani Banda, mkuu wa zamani wa nchi hiyo atachuana vikali na Rais wa sasa, Peter Mutharika. Banda anafahamika kwa kutoa misaada kwa maskini nchi nzima.
Chama tawala cha Democratic Progressive Party (DPP) kimesema kitatii sheria kama ilivyo kwa sheria nyingine za nchi hiyo.
Chama cha United Transformation Movement (UTM) kinachoongozwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima ambaye amevunja uhusiano na Mutharika, amesema: "Tulihitaji sheria hii jana,” akimaanisha ilipaswa kuwapo tangu awali.