Ndege za Marekani zachochea uhasama Korea Kaskazini, Kusini

SEOUL, Korea Kusini. Korea Kaskazini imeijia juu Korea Kusini kwa mpango unaoendelea wa kununua ndege za kivita kutoka Marekani ikisema itajibu mapigo kwa kutengeneza na kufanya majaribio makombora ya kuzitungua.

Taarifa ambayo pia imeitaka Korea Kusini kuachana na mpango huo wa ajabu, imekuja katika kipindi ambacho mkutano kati ya Rais Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un ukidhaniwa utarejesha majadiliano baina ya nchi hizo.

Katika manunuzi hayo yanayoaminika kuwa ni makubwa zaidi, Korea Kusini inataka kununua ndege 40 za kivita aina ya F-35 kutoka Lockheed Martin ifikapo 2021.

Kwa mujibu wa maofisa wa Kosea Kusini ndege mbili za kwanza zinatakiwa kuwasilia nchini humo Machi na nyingine mbili wiki kadhaa baadaye.

Mradi huo ulitangazwa mwaka 2014 ili nchi hiyo iweze kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka kutoka Korea Kaskazini ambayo imekuwa inafanya majaribio mengi ya makombora.

Uhasama ulikuwa unapungua taratibu tangu mwaka jana pale Korea Kaskazini na  Marekani zilianza majadiliano kuhusu nyuklia, lakini Korea Kusini iliendelea mpango wa manunuzi uliokuwa tayari umepitishwa.

Leo Alhamisi, Waziri wa mambo ya nje  wa Korea Kaskazini alitoa taarifa ya malalamiko, akisema awamu ya pili ya ndege hizo itawasili Korea Kusini katikati ya Julai, jambo ambalo maofisa wa Seoul hawakuthibitisha.

Serikali ya Korea Kusini haikujitokeza kujibu shutuma za jirani yake, lakini Ofisa manunuzi wa silaha amesema mpango huyop unaendelea kama ulivyopangwa na kuwa ndege 10 kati ya 40 zinatakiwa kuwasilia kufikia mwisho mwa mwaka huu.