Polisi wamuhoji mbunge mauaji ya mwandishi Ghana

Muktasari:

  • Mwandishi huyo wa habari alishiriki katika uchunguzi ambao uliibua kashfa ya rushwa katika soka barani Afrika na kusababisha viongozi, waamuzi na maofisa wa mchezo huo maarufu duniani kujiuzulu.

Accra. Mwanasiasa wa Ghana, ambaye aliahidi kumlipa mtu yeyote ambaye atamshambulia mwandishi wa habari za uchunguzi, amehojiwa ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa kifo cha mwanahabari huyo, polisi wametangaza.
Ahmed Hussein-Suale, ambaye alifanya uchunguzi wa habari za rushwa katika soka barani Afrika, aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akirejea nyumbani kwake jijini Accra wiki iliyopita.
Mauaji hayo yalishtua sehemu kubwa ya Ghana, ambayo inajitangaza kuwa na demokrasia imara katika kanda ambayo haina utulivu na ambayo vyombo vya habari vina uhuru mkubwa.
Msemaji wa polisi, David Eklu alisema katika taarifa yake juzi kuwa wapelelezi wameanza uchunguzi mkubwa wa kifo cha mwandishi huyo.
"Timu ya wachunguzi na wataalamu wengine imemuhoji Kennedy Agyapong, mbunge kutoka Jimbo la Kati la Assin, walichukua maelezo yake," alisema.
Jina la Agyapong lilitajwa ikiwa ni sehemu ya kuanika rushwa hiyo. Baadaye alikwenda kituo cha televisheni, akaonyesha picha za Hussein-Suale na kusema atamlipa mtu yeyote ambaye amemshambulia.
Hata hivyo, amekanusha kwamba aliratibu mauaji hayo na kwamba hajawahi kufanyiwa mabaya na Hussein-Suale.
Lakini ameendelea kumpinga mwandishi huyo pamoja na Anas Aremeyaw Anas, ambaye ni bosi wake katika kampuni iliyofanya uchunguzi huo.
"Dhambi ambayo wamekuwa wakifanya itawafuata," alisema Agyapong, ambaye ni mwanachama wa chama cha New Patriotic Front cha rais wa sasa, Nana Akufo-Addo.
Anas, ambaye anaficha sura yake anapokuwa hadharani kwa kuvaa kofia tofauti na vitambaa, pia ametishiwa kuuawa.
Polisi imetangaza dau la dola 3,000 (sawa na zaidi ya Sh6 milioni za Kitanzania) kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa walioshiriki katika mauaji na kukutwa nna hatia.
Habari hiyo ya uchunguzi ilisababisha kujiuzulu kwa kiongozi wa Chama cha Soka cha Ghana na kufungiwa kwa zaidi ya waamuzi 12, waamuzi wasaidizi na maofisa wengine.