Taharuki ajali ya ndege Ethiopia, Mashirika mengi yafuta safari za Boeing 737 MAX 8, yasitisha ununuzi

Dar es Salaam. Hofu juu ya matumizi ya ndege za Boeing 737 Max 8 imeibuka baada ya ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines iliyoua watu 157, ikiwa ni takriban miezi mitano tangu ndege ya aina hiyo kuanguka nchini Indonesia.

Ndege ilikuwa mpya, hali ya hewa ilikuwa safi na marubani walikuwa wakijaribu kuirejesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole. Hawakufanikiwa. Kuna kitu hakikuwa sawa.

Jana, China iliamuru mashirika yote ya nchi hiyo kusimamisha safari za ndege za aina hiyo, na kufuatiwa na Indonesia na baadaye shirika hilo la Ethiopian Airlines kutokana na ajali hiyo iliyotokea muda mfupi baada ya kupaa kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa kuelekea Nairobi.

Watu kutoka mataifa 35 walipoteza maisha, ikiwa ni miezi michache baada ya ndege ya Lion Air ya Indoneasia kuua watu 189 dakika 13 baada ya kupaa.

Ndege hiyo ya Ethiopian Airlines, shirika kubwa barani Afrika kwa usafiri wa anga, ilikuwa na miezi minne tangu inunuliwe kabla ya kupata ajali hiyo Machi 10.

Wakati vifaa viwili vya kurekodi taarifa za ndege na sauti (Digital Flight Data Recorder na Cockpit Voice Recorder) vikiwa vimepatikana, mjadala mkubwa uliotawala dunia jana ni kuhusu matatizo ya kiufundi ya ndege hiyo ambayo wachunguzi wanahisi yanaweza kuwa ndiyo yanayochangia ajali zake.

Mjadala huo ulijikita katika mfumo wa kompyuta unaoiwezesha Boeing 737 Max 8 kukabiliana na matatizo, wakisema inaweza kuwa ndio chanzo cha ajali hiyo.

John Nyamwihura, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama wa ndege nchini, alifananisha ajali hiyo na ya Lion Air, akisema pamoja na taarifa rasmi ya ajali hiyo kutotoka, chanzo kinaweza kuwa mfumo huo wa kompyuta.

“Kutokana na tukio lililopita uchambuzi uliofanyika unaonyesha kuwa ndege hizo zimejengewa na mitambo ya kompyuta inayolinda au kusahihisha makosa ya rubani wakati wa kupaisha ndege au kugeuza kwa kuwa ajali nyingi zinatokana na makosa kama hayo ya rubani,” alisema Nyamwihura.

Alisema awali marubani walikuwa wakizidisha kiwango cha kupaa au kugeuka, hivyo ndege ilikuwa inajikuta ikidondoka. Lakini mfumo huo ulikuja kutatua tatizo hilo kwa kuwa unazuia makosa hayo ya rubani.

“Mfumo huo wa kompyuta hiyo inasahihisha makosa ya rubani lakini inapopata hitilafu, inamkosoa rubani hata kama hajakosea. Kwa hiyo unakuta anaielekeza juu, kompyuta inaelekeza chini hivyo hawezi kuiongoza tena na hicho ndicho kilichotokea Indonesia,”

Alisema ubaya ni kuwa Boeing hawakuwapatia mafunzo marubani kuhusu namna ya kukabiliana na dharura ya namna hiyo kwa kuwa katika mwongozo wa marubani wa ndege hiyo hakuna namna ya kuzima mfumo huo ili mtu aiendeshe mwenyewe.

“Haya mambo yanatokea wakati mtu ndiyo anaanza kupaa hata rubani akisema aitulize wakati anahangaika kidogo anakuta tayari ndege imekwishalamba mchanga. Ndege hiyo ni ya kisasa lakini mifumo ambayo imewekwa ndiyo imeanza kuleta matatizo,”

Alisema wakati ndege hizo zinarushwa bila mfumo huo wa kompyuta zilikuwa salama kwani Boeing 737 imekuwepo tangu mwaka 1965 kabla hazijaboreshwa kuwa 737 Max (mwaka 2011) na zimetumiwa na mashirika tofauti.

Marubani wa baadhi ya mashirika wakiwemo wa American Airline na Southwest, waligoma wakisema hawajawahi kutaarifiwa kuhusu mfumo mpya ambao ndege inaweza kuelekeza pua yake chini kutokana na taarifa za sensor.

Alan Diehl, mchunguzi wa zamani wa usafiri wa anga nchini Marekani, aliiambia tovuti ya Market Watcher kuwa kufanana kwa ajali hizo mbili ni katika marubani wote kujaribu kushughulikia tatizo na kasi ya ndege wakati wa kupaa, “jambo linaloonyesha wazi kuwa kuna uwezekano wa tatizo la kuidhibiti”.

Lakini Diehl alisema kuna uwezekano wa matatizo mengine kama uzito wa mzigo, tatizo kwenye injini, makosa ya rubani, hujuma au ndege uwanjani.

Alisema Ethiopian Airlines ina sifa nzuri, lakini wachunguzi wataangalia matengenezo ya ndege, hasa kwa kuwa tatizo hilo linaweza kuwa ndilo lililochangia ndege ya Lion Air.

Kampuni ya Flightradar inayofuatilia urukaji wa ndege kupitia akaunti yake ya Twitter ilisema kuwa mwendo wa ndege hiyo wakati wa kupaa ulikuwa ukibadilikabadilika.

Tatizo la mfumo huo wa kompyuta liliwahi kudokezwa na kampuni ya Boeing baada ya ajali ya Indonesia. Ripoti yake ilionyesha kuwa kabla ya kuanguka rubani alifanya jitihada kubwa kuongoza ndege hiyo bila mafanikio.

Boeing walisema wakati mwingine king’amuzi (sensor) cha mfumo wa ndege hiyo kinaweza kutoa ishara zisizo sahihi na kusababisha mfumo huo kuchukua hatua ambayo haihitajiki, hivyo marubani wanapaswa kuangalia kitabu cha mwongozo linapotokea tukio kama hilo.

Boeing imetuma wataalamu wake nchini Ethiopia kuchunguza ajali hiyo na rais wa kampuni hiyo, Dennis Muilenburg alisema wameichukulia ajali hiyo kwa uzito na kujifunza ili kuboresha usalama wake.

“Kila siku mamilioni ya watu hutegemea ndege zetu za kibiashara kusafiri kote ulimwenguni kwa njia salama. Wakati hili halifanyiki sisi huchukulia hali hiyo kwa uzito,” alisema.

Ndege hizo zimekuwa maarufu na zenye soko kubwa hasa kutokana na teknolojia ya kisasa iliyowekwa ndani yake pamoja na matumizi mazuri ya mafuta, ikishindana na ndege za Airbus.

Safari za 737 Max 8 zasitishwa

Umaarufu huo umefanya mashirika kadhaa kumiliki Boeing 737 Max 8 kama Norwegian Air, Air China, TUI, Air Canada, United Airlines, American Airlines, Turkish Airlines, Icelandair, Cayman Airways na FlyDubai.

Cayman Airways nao wamezuia ndege zao za aina hiyo kufanya safari.

Hata hivyo kampuni ya ndege ya Southwest Airline , IcelandAir, shirika la ndege la Thailand, wamesema hawana shaka na usalama wa ndege hizo na wataendelea kuzitumia katika safari zao mbalimbali.