Tshisekedi aenda Rwanda

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi

Muktasari:

  • Ni ziara yake ya kwanza nchini humo tangu achaguliwe kuwa Rais wa DRC

Kinshasa, DRC. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi, yuko Rwanda na leo ametembelea eneo la kumbukumbu la mauaji ya kimbari jijini Kigali.

Ziara hii imekuja, wiki mbili kuelekea maadhimisho ya miaka 25 tangu kutokea kwa mauaji hayo ya kimbari ya mwaka 1994 ambayo yalisababisha zaidi ya watu 800,000 kupoteza maisha.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Rais Tshisekedi baada ya kuchaguliwa kuwa rais wa DRC.

Rwanda na DRC ni mataifa jirani ambayo yanashirikiana kibiashara lakini suala la usalama mipakani linaendelea kuwa  changamoto kwa muda mrefu sasa.

Kwa upande mwingine Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ameishtumu Uganda kwa kuiwekea vikwazo vya kufanya biashara, suala ambalo amesema linakwenda kinyume na makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kagame ameishutumu Uganda, kwa kuzuia bidhaa kutoka Rwanda kwa sababu ambazo amezieleza kuwa hazina uzito na hivyo kuharibu biashara.

Kagame amelalamikia mizigo ya nchi yake inayotokea Bandari ya Mombasa kuzuiwa kwa zaidi ya miezi mitano, sawa na maziwa yaliyokua yanakwenda Kenya kuzuiwa kwa siku kadhaa na kuharibika, suala ambalo amesema ni siasa.