Tshisekedi atangazwa Rais DRC

Sunday January 20 2019

 

Kinshasa,DRC. Mahakama ya Kikatiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  imemtangaza Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini humo.

Mahakama hiyo iliyatupilia mbali madai ya  Kiongozi wa Upinzani Martin Fayulu kwamba uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu.

Fayulu anadai kwamba Tshisekedi na Rais Joseph Kabila walifanya mpango wa siri baada ya matokeo ya awali kuonesha kwamba mgombea ambaye alikuwa akiungwa mkono na Kabila, Emmanuel  Shadary, kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo.

Kuapishwa wiki ijayo

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la DW ,uamuzi huo wa mahakama unamaanisha kuwa sasa Tshisekedi anaweza kuapishwa kuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumanne wiki ijayo.

Fayulu ameitaka jumuiya ya kimataifa kupinga ushindi huo wa Tshisekedi kwa kutotambua mamlaka yake aliyoyataja yasiyoungwa mkono na DRC.

Vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa viliripoti kuwa data zilizovujishwa za uchaguzi huo zilionesha kuwa Fayulu ndiye aliyeshinda na sio Tshisekedi.

 

Kanisa lenye ushawishi mkubwa nchini humo la Kikatoliki pia limeunga mkono hoja ya Fayulu kuwa Tshisekedi hakushinda katika uchaguzi huo wa Desemba 30 na Umoja wa Afrika ulitaka matokeo kamili ya uchaguzi huo wa Rais kucheleweshwa.

Nchi za magharibi zagoma kutuma pongezi

Nchi za magharibi bado hazikumtumia pongezi Tshisekedi, na Ufaransa imeeleza wasiwasi wake juu ya matokeo rasmi ya uchaguzi, ambayo yamempatia ushindi Tshisekedi kwa asilimia 38.57 ya kura zote zilopigwa na Fayulu kupata asilimia 34.8.

Gazeti la Financial Times na vyombo vengine vya habari vya kimataifa vimethibitisha kuona nyaraka zinazosema kuwa Fayulu ndiye mshindi wa uchaguzi huo.

Kambi ya Fayulu iliusifu Umoja wa Afrika kwa kutoa ombi la kutaka matokea ya mwisho yaahirishwe, lakini kambi ya Tshisekedi hauikufurahishwa.

Mvutano huo umezua wasiwasi kwamba mgogoro wa kisiasa ulioanza mara baada ya Rais Joseph Kabila kukataa kuachia madaraka mwishoni mwa muhula anaoruhusiwa kikatiba kumalizika miaka miwili iliyopita unaweza kusababisha umwagaji damu.

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika-SADC, ambayo inajumuisha Angola na Afrika Kusini awali ilitoa wito wa kura kuhesabiwa tena pamoja na kuundwa kwa Serikali ya umoja wa muungano.

Lakini taarifa yake ya baadaye, haikutaja madai hayo, badala yake iliwatolea wito wanasiasa wa Congo "kushughulikia malalamiko yoyote ya uchaguzi kwa mujibu wa  Katiba ya nchi hiyo na sheria husika za uchaguzi".

Advertisement